Habari

Chiloba wa LGBTQ alipanga kuokoka na kuacha ushoga kabla kuuawa kinyama

Na TITUS OMINDE December 18th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MWANAHARAKATI wa ushoga na usagaji Edwin Kiprotich Kiptoo maarufu Chiloba alikuwa amedokezea familia yake kwamba aliazimia kuokoka na kuachana na ushoga mkesha wa mwaka mpya 2023, kabla kuishia kuuawa na mpenziwe wa kiume Jacktone Odhiambo.

Gaudensia Tanui ambaye ni binamu wa marehemu aliambia Mahakama Kuu ya Eldoret kwamba Chiloba alikuwa ameweka wazi nia yake ya kuasi maisha ya kutetea mashoga na wasagaji (LGBTQ) na badala yake kuanza kutetea injili ya dini ya kikristo.

“Marehemu alikuwa ameniambia kuwa alitaka kuokoka mwaka mpya na kuasi maisha yake ya kale ili aanze mapya kama mkritso. Kuawa kwake kulizima ndoto yake hiyo ya kuokoka,” alisema Tanui  na kueleza korti kwamba mshtakiwa Jacktone Odhiambo alistahili hukumu ya kifo baada ya kupatikana na hatia.

Akitiririkwa na machozi mbele ya Jaji Reuben Nyakundi, Bi Tanui alisimulia jinsi marehemu alikuwa kijana mzuri mwenye tabia njema katika familia yao huku akilaumu Bw Odhiambo kwa kuharibu hatima ya mwendazake.

Jackton Odhiambo (kati), aliyeshtakiwa kwa kumuua Edwin Kiprotich Kiptoo maarufu Chiloba, akizungumza na wakili wake Sammy Mathai (kushoto) katika Mahakama Kuu ya Eldoret kabla kutolewa kwa hukumu dhidi yake mnamo Desemba 16, 2024. PICHA | JARED NYATAYA

Bi Tanui aliongeza kwamba Chiloba alikuwa kijana wa pekee na alipendwa na kila mtu katika familia yao.

Akitoa hukumu Jaji Nyakundi  aligusia suala la wanaume wa kiafrika kuwa na mahusiano ya kimapenzi baina yao.

“Chembechembe za nguvu za kiume zilizopatikana sehemu nyeti za marehemu ziliashiria uovo ulivyo katika jamii. Kama Waafrika hatutambui ndoa baina ya wanaume, hii ni tabia mbaya,” akasema Jaji Nyakundi.

Jaji huyo alisema mshtakiwa alistahili hukumu ya kunyongwa ila hukumu hiyo imezuiwa kutekelezwa tangu Mahakama ya Upeo iiharamishe mwaka 2017.

“Kumetokea hisia mseto kuhusu hukumu ya kunyongwa, huenda hii ndio imechangia ongezeko la visa vya watu kuuwana kiholela. Kuna haja ya kutathmini upya hukumu,” alihoji Bw Nyakundi.

Alimpa Bw Odhiambo kifungo cha miaka 50 jela baada ya kupatikana na hatia ya kumuua Chiloba.

Jeneza lenye mwili wa Edwin Kiprotich maarufu Chiloba wakati wa mazishi yake nyumbani kwao Sergoit, Kaunti ya Elgeyo Marakwet, mnamo Januari 17, 2023. PICHA | JARED NYATAYA

Bw Odhiambo, hata hivyo, alikuwa amekana kumuua Chiloba ndani ya nyumba yao eneo la Chebisaas katika Kaunti Ndogo ya Moiben, Kaunti ya Uasin Gishu.

Kisha baadaye akasafirisha mwili huo uliokuwa umeanza kuoza kwa sanduku la mabati na kuutupa ulikopatikana Januari 3, 2023 kwenye barabara ya Kipkenyo-Kaptinga eneo la Kapseret yapata kilomita 10 kutoka katikati mwa jiji la Eldoret.