Gachagua ampa Kalonzo sharti kali kabla ya kumuunga 2027
KIONGOZI wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka atalazimika kuongeza mara mbili kura katika ngome yake ya Ukambani ili kufuzu kuungwa mkono na eneo la Mlima Kenya kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2027, aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua alisema jana.
Bw Gachagua alisema kura milioni mbili za sasa za Ukambani hazitoshi kumpeleka Bw Musyoka Ikulu.
“Uongozi na siasa ni kuhusu idadi. Mnahitaji kujiandikisha kama wapiga kura. Nataka niwape changamoto mjue mkitaka tuwe pamoja serikalini lazima mjisajili vijana wote kupiga kura. Msisubiri hadi dakika ya mwisho. Msajili muwe na kura za kutosha. Mkishapata kura 3.5 milioni hadi milioni nne, nitafuteni. Katika eneo la Mlima Kenya, tumejipanga kuongeza idadi yetu hadi kura milioni 10,” akasema.
Bw Gachagua alizungumza katika Shule ya Upili ya Kyanguyu katika Kaunti ya Makueni wakati wa mazishi ya Agnes Mwikali Muia, mamake Askofu Francis Mulinge,
mwenyekiti wa kitaifa wa Muungano wa Wahubiri Kenya. Uhusiano kati ya jamii ya Kamba na Mlima Kenya ulitawala mazungumzo katika sherehe hiyo.
Washirika wa Bw Gachagua na wale wa Bw Musyoka walitaka viongozi hao wawili kuungana na kufanya kazi pamoja kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2027. Huku wakimkashifu Rais William Ruto, wanasiasa wa kambi hizo mbili waliafikiana kuwa Bw Musyoka atakuwa mgombeaji urais 2027.
Akimrushia vijembe bosi wake wa zamani ambaye alimshtumu kwa kufumbia macho shida za Wakenya, Bw Gachagua aliongoza wito wa Bw Musyoka kukata uhusiano wake na kiongozi wa ODM Raila Odinga na kuungana na viongozi wa Mlima Kenya.
“Tunazungumza na Kalonzo na Wakenya wengine kama vile Eugene Wamalwa na wengine katika maeneo mengine ya nchi. Tunazungumza kama Wakenya kutafuta njia ya kuinua uchumi wetu na kumaliza utamaduni wa uwongo nchini Kenya. Tunataka kuipeleka Kenya mbele. Jinsi (Mbunge wa Githunguri Gathoni) Wamuchomba atakavyowaambia, hatushirikiani na watu wa kushindwa. Popote utakapotuona, hiyo itakuwa timu ya kushinda. Kwa kuwa tumekubali kuungana, sisi ndio timu itakayoshinda,” Bw Gachagua alisema.
Seneta wa Makueni Daniel Maanzo alimweleza Bw Gachagua kwamba jamii ya Wakamba iko tayari kuunga mkono jamii ya Mlima Kenya katika azma yake ya baadaye ya kisiasa iwapo itamuunga mkono Bw Musyoka.
Mkewe Bw Gachagua, Askofu Dorcas Rigathi, alijiunga na makasisi na wanasiasa waliokuwepo kumkashifu Rais Ruto. Alijuta kuwa miongoni mwa wahubiri waliompigia kampeni Rais Ruto.
“Tumelaumiwa kwa kuhubiri na kuwaambia Wakenya kwamba utawala wa Kenya Kwanza ungekuwa wa kimaendeleo na sio wa kuharibu. Tunaomba radhi kwa sababu unapokutana na mtu hauwezi kujua tabia yake,” alisema.
Alikuwa akimjibu aliyekuwa Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu ambaye alikuwa amewaonya wahubiri dhidi ya “kuwapotosha Wakenya tena”.