Habari za Kitaifa

Mkenya aliyezuiliwa na Amerika miaka 17 hatimaye aachiliwa huru

Na BRIAN OCHARO December 19th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

RAIA wa Kenya, Mohamed Abdul-Malik Bajabu, hatimaye ameachiliwa huru kutoka kambi ya kijeshi ya Amerika iliyo Guantanamo Bay, Cuba, ambako alikuwa amezuiliwa kwa miaka 17.
Wizara ya Ulinzi ya Amerika ilitangaza Jumanne usiku kuachiliwa kwa Bw Bajabu kutoka kwa kifungo cha miaka 17 bila kufunguliwa mashtaka.

Kuachiliwa kwake kulifuatia uamuzi wa Bodi ya Ukaguzi wa Mara kwa Mara ya Marekani (PRB), ambayo iliamua kwa pamoja kumrejesha nchini mwake.

Familia yake inayoishi Kenya imeeleza kuridhishwa na hatua hiyo lakini ikaomba muda wa kupanga mambo yao kabla ya kuzungumza na vyombo vya habari.

Mmoja wa jamaa zake aliyezungumza na Taifa Leo kwa sharti la kutotajwa jina kutokana na uzito wa suala hilo, alisema wanaishukuru serikali ya Kenya Kwanza kwa kuingilia kati.

Duru katika familia zilisema, hasa, wanathamini juhudi za Rais William Ruto na Waziri wa Masuala ya Kigeni Musalia Mudavadi. Hata hivyo, familia iliomba kwamba vyombo vya habari viwape muda kabla ya kutoa maelezo zaidi kuhusu hatua zitakazofuata.

“Vyombo vya habari vimekuwa nasi katika safari hii yote. Siwezi kukunyima nafasi ya mahojiano, lakini tafadhali turuhusu tupange baadhi ya mambo. Hata hivyo, nitazungumza na vyombo vya habari,” jamaa wa Bajabu aliambia Taifa Leo.

Bajabu alikuwa mfungwa pekee raia wa Kenya aliyekuwa amezuiliwa Guantamo Bay, ambayo ni kambi ya kijeshi ya Amerika nchini Cuba inayotumika kuwazuilia watu wanaoshukiwa kuwa wanamgambo na magaidi waliokamatwa na majeshi ya Amerika.

Kundi la kutetea haki za wafungwa la Reprieve limeeleza kuridhishwa na hatua ya kuachiliwa kwa Bajabu, likisema kwamba hatua hiyo ilikuwa imesubiriwa kwa muda mrefu zaidi.

“Kile kidogo zaidi ambacho Serikali ya Amerika inaweza kufanya, baada ya kumfunga Bajabu bila kufunguliwa mashtaka kwa miaka 17, ni kuhakikisha kwamba huu ni mwisho wa mateso yake na mwanzo wa maisha mapya na familia yake,” Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Reprieve, Dan Dolan, alisema katika taarifa kwa vyombo vya habari. Mawakili wake wakiongozwa na Frank Panopoulos, walitoa kauli sawa na hiyo.

“Watoto wake walikuwa wachanga alipoteswa, kuhojiwa na kusafirishwa hadi Guantanamo, na sasa wamekua. Deni hilo kamwe haliwezi kulipwa, lakini cha chini kabisa ambacho Marekani inaweza kufanya ni kuhakikisha kwamba Abdulmalik anapata msaada na nafasi anayohitaji ili kuanza maisha yake upya,” akasema.