Jamvi La Siasa

Baada ya kusukuma chanjo ya Covid-19, Kagwe arejeshwa kuvumisha chanjo ya mifugo

Na FRIDAH OKACHI December 20th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

ALIYEKUWA Waziri wa Afya katika serikali ya Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta Bw Mutahi Kagwe, ameteuliwa kuwa Waziri wa Kilimo na Ustawishaji Mifugo.

Kwa uteuzi huu, inamaanisha kwamba akiidhinishwa na Bunge, Bw Kagwe anatarajiwa kusukuma chanjo ya mifugo baada ya kusukuma wananchi kupata chanjo ya corona alivyofanya 2020-2021.

Taarifa iliyotiwa sahihi na Mkuu wa Utumishi wa Umma Bw Felix Koskei, Alhamisi Desemba 19, 2024, ilisheheni mabadiliko na teuzi za nyadhifa za juu katika serikali kuu.

“…Uteuzi uliofanywa unahusiana na watu watakaohudumu katika nafasi za juu katika sera za taifa; unahusisha Baraza la Mawaziri pamoja na Mashauri ya Kigeni,” ilisema taarifa hiyo.

Bw Kagwe alipata umaarufu wakati wa janga la corona, kwa kuwa mstari wa mbele kutoa taarifa za kila siku kuhusu hali ya maambukizi ya COVID-19 nchini, hatua zilizochukuliwa, na miongozo ya kudhibiti ugonjwa huo. Hotuba zake zenye mamlaka na ufafanuzi wa kina zilimpa nafasi ya kuwa sura ya juhudi za serikali dhidi ya janga hilo.

Wakati huo alionekana kuwa kiongozi na msimamo dhabiti. Alisisitiza mara kwa mara umuhimu wa kuvaa barakoa, kunawa mikono, na kuzingatia umbali wa kijamii.

Maneno yake kama “if you treat this disease normally, it will treat you abnormally” yalipata umaarufu mkubwa, na hata kutumika kama nukuu mashuhuri.

Ana uzoefu katika utumishi wa umma na uelewa wa siasa za nchi, kwa kuwa aliwahi kuwa seneta katika mwaka 2013 hadi 2017.

Zaidi ya hayo, wakati wa serikali ya Rais Mwai Kibaki, Kagwe alishiriki jukumu muhimu katika kuboresha sekta ya mawasiliano, hatua ambayo iliongeza sifa zake kwa uwezekano wa kurejea katika Baraza la Mawaziri.

Uteuzi huo, huenda ukasaidia kuziba pengo kati ya makundi tofauti ya kisiasa, hasa kufuatia mivutano ya hivi karibuni ndani ya serikali.

Katika uteuzi wa Rais, aliyekuwa Gavana wa Kiambu Bw William Kabogo ametauliwa kuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano, na Uchumi wa Kidijitali.

Aliyekuwa Gavana wa Nakuru, Bw Lee Kinyanjui, ameteuliwa kuwa Waziri wa Uwekezaji, Biashara, na Viwanda, nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Salim Mvurya, ambaye amehamishwa hadi katika Wizara ya Michezo ambayo imekuwa wazi kufuatia uteuzi wa Kipchumba Murkomen kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani.