Afueni kwa wandani wa Kiraitu kuhusu udhibiti wa chama cha ‘Mbas’
WANDANI wa aliyekuwa Gavana wa Meru Kiraitu Murungi wamepata afueni baada ya Mahakama ya Rufaa mjini Nakuru kusitisha, kwa muda, utekelezaji wa agizo la awali la kuzima kuchapishwa kwa majina ya maafisa wapya wa chama cha Devolution Empowerment Party (DEP).
Majina ya maafisa hao yalitarajiwa kuchapishwa katika Gazeti Rasmi la serikali Mei mwaka huu, 2024.
Mwezi Oktoba, Mahakama Kuu ya Kericho ilibatilisha kufurushwa kwa wakili Mugambi Imanyara kama Katibu Mkuu wa DEP.
Bw Imanyara, aliagizwa kuitisha Kongamano maalum la Wajumbe wa Kitaifa (NDC) kuchagua maafisa wa kitaifa wa chama hicho.
Uamuzi huo ulitoa nafasi kwa Bw Imanyara kudhibiti usimamizi wa chama hicho na kuwaondoa wandani wa Murungi kutoka uongozi wa chama cha DEP.
Novemba 2024, Bw Imanyara aliongoza kongamano maalum la NDC ambako alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu pamoja na maafisa wengi.
Hata hivyo, Kamati Kuu ya Kitaifa (NEC) ya chama hicho ilielekea katika Mahakama ya Rufaa ikidai Mahakama Kuu ilikosea kwa kuharamisha majina ya maafisa wa chama kulingana na notisi ya Gazeti Rasmi la serikali nambari 5805 la Mei 2024.
Wanachama wa DEP pia waliwasilisha kesi katika Jopo la Kutatua Mizozo kati ya Vyama vya Kisiasa (PPDRT) na likazuia maafisa wa muda, waliochaguliwa, kuanza kutekeleza majukumu yao.
Katika rufaa yao, wanachama hao na NEC walikosoa uamuzi uliotolewa na Jaji Joseph Sergon kwa kile walisema ni kuingilia wajibu wa PPDRT.
“Kwa kuamua Katiba ilikiukwa wakati wa uchapishwaji wa majina ya maafisa, shughuli za chama cha DEP zimelemazwa na haiwezi kutoa pesa kutoka kwa akaunti zake ili kulipa mishahara wala kulipia mahitaji ya afisi. Hii ni kwa sababu hamna maafisa wanaoruhusiwa kuendesha shughuli za chama,” walalamishi wakasema.
Mnamo Ijumaa majaji wa Mahakama ya Rufaa Mohamed Warsame, John Mativo na Paul Mwaniki walikubaliana na wakata rufaa hao na kusitisha utekelezaji wa agizo la Mahakama Kuu lililotolewa Oktoba 2024.