MAONI: 2025 heri Afrika ijipange kwa sababu hakuna atakayeshughulika na matatizo ya bara hili
MWAKA huu unamwishia Mwafrika vibaya. Dunia imemzoea hivi kwamba masaibu yanayomsibu, hasa ya vita na njaa, hayajadiliwi kama dharura tena.
Ukiwasikiliza watu wa asili za mabara mengine wakizungumza kuhusu mabadiliko wanayotarajia mwakani, hasa baada ya Donald Trump kuapishwa ili kuanza muhula wake wa pili kama rais wa Amerika, hawataji taifa lolote la Afrika kama mojawapo ya yanayohitaji kushughulikiwa kwa dharura.
Ukimuuliza Mzungu ni suala gani ambalo angetaka lipewe kipaumbele tunapoingia mwaka mpya wa 2025, atatamka ‘Ukraine’ mara moja bila kupepesa jicho.
Aliye na ufahamu zaidi atakwambia kuwa Mashariki ya Kati inapaswa kuangaliwa kwa jicho la tatu kwa kuwa Israel, Palestina na Lebanon wanauana kwa jinsi isiyostahili.
Hakuna anayekwambia kuwa Sudan imekuwa vitani kwa miaka kadha sasa, haijawa na serikali rasmi, majeshi yanauana na kuangamiza raia kijijini, nao raia wanaosazwa na mtutu wa bunduki wanakufa njaa.
Sudan Kusini, taifa ambalo ni tajiri wa madini ila linaloishi kwa msaada wa mataifa fadhili, limeongozwa na serikali ya mpito kwa miaka kadha, chaguzi zikiahirishwa kiholela, wala hakuna anayejituma kutafuta suluhisho la kudumu.
Hata msukosuko ambao umezuka nchini Msumbiji kutokana na matokeo y uchaguzi wa urais haumkoseshi mtu usingizi, hasa kwa kuwa ni wa kisiasa na, labda, Waafrika tumezoeleka kuvaana wazima-wazima kila matokeo ya uchaguzi yanapotangazwa.
Msumbiji patatamkwa neno pale matatizo ya kisiasa yatakapokutana na yale ya kigaidi. Hapo ndipo mafedha yatakapomwagwa, labda hata Umoja wa Mataifa ujadili hali hiyo, Afrika ikumbukwe kwa kuwa matatizo yake yanatishia usalama wa mataifa yaliyoendelea.
Masaibu hayo yote yangekuwa barani Uropa au Amerika, suluhu ya dharura ingetafutwa ili kiwango cha ubora wa maisha kisishuke, watu wasiteseke sana.
Dunia imeikatia tamaa Sudan na kuipuuza kwa urahisi kwa kuwa hakuna uwezekano wa vita hivyo kuenea hadi Uropa wala kuliathiri bara hilo kwa vyovyote vile.
Misaada ya kibinadamu ambayo hutolewa kwa dharura nchi inaponuka baruti haipelekwi huko, kwa hivyo baadhi ya watu wanakufa njaa na wengine kwa kukosa matibabu.
Hatujasikia visa vya wahisani kuhatarisha maisha yao na kwenda eneo la vita nchini Sudan; hayo tumeyasikia Gaza na Lababon. Kimsingi hakuna aliye radhi kufa akitusaidia.
Nimeona michango mingi sana ikifanywa mtandaoni kwa ajili ya kuwalisha na kuwavisha raia wa Ukraine tangu Urusi ishambulie nchi yao.
Na watu wanachanga kila siku kwa sababu vita hivyo vingali vinaendelea.
Nchini Amerika, wapo pia waliojasiria kutundika bendera za Ukraine kwenye magari yao binafsi ili kuonyesha kuwa wanafungamana na raia wa taifa hilo wakati huu wa mahangaiko.
Sijaona mchango wowote unaolenga kumsaidia raia wa Sudan, wala taifa jinginelo la Afrika, ambaye anataabika akisubiri pepo wa mauti amjie.
Nahuzunikia hali hii sana kwa kuwa Afrika kuna matajiri wengi na wanaharakati wa haki za binadamu ambao wana ubia na mataifa yaliyoendelea.
Hata bila kuyaombea misaada mataifa ya Afrika ambayo yamegubikwa na mizozo, Waafrika wenyewe wanaweza kuanzisha michango na kampeni za kuishinikiza dunia kuingilia kati mizozo hiyo ili raia waache kuteseka.
Tunasubiri Wazungu walete misaada ili tuigawie masaibu yetu, hatutaki kuchoka. Tumekuwa wazembe hivi kwamba hata jitihada za kudhibiti hali kuliko na matatizo zinafadhiliwa na mataifa yaliyoendelea, na yakisitisha ufadhili huo tunarudi nyumbani kusubiri waghairi nia.
Hivi hatuwezi kuwa na juhudi za kuleta amani Afrika bila kutegemea posho kutoka kwa mabwana hao? Na ikitokea kwamba wao ndio wafadhili wa vita hivyo barani, hatutawahi kupata suluhisho. Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) haitawahi kuwa na amani kamwe?
Afrika inakaa kama maskini ambaye akiingia mkahawani na matajiri anachaguliwa atakachokula kwa sababu hana uwezo wa kujinunulia chochote.
Tumetegemea nundu kwa muda mrefu mno, hebu na tuanzishe juhudi za kuleta amani kote barani bila kuwategemea watu ambao labda raha yao ni kuona tukitengana.