Teknolojia asilia anazotumia kufufua hadhi ya shamba, kuongeza mazao
KIJIJI cha Shembekho, Matungu, Kaunti ya Kakamega, unapokizuru wakazi wengi wamezamia kilimo cha mahindi na maharagwe.
Hata hivyo, katika shamba la Rosemary Okello mambo ni tofauti.
Kando na mahindi na maharagwe, ana mseto wa matunda kama vile maparachichi, mapera, ndizi, maembe na mapapai.
Isitoshe, mama huyu ambaye amekuwa akiendeleza kilimo kwa zaidi ya miaka 15, hukuza mboga za kienyeji kama vile sucha – maarufu kama managu, mchicha (terere), kunde, kansara na saga.
Vilevile, analima viazi vitamu, nduma na soya.
Rosemary anasema maendeleo hayo yanatokana na teknolojia asilia alizokumbatia.
“Teknolojia za kurejesha (regenerative technologies), ni mbinu asilia kuendeleza kilimo ambazo tukizikumbatia zitasaidia kuboresha shughuli za kilimo,” anasema.
Mbinu hizo zinajumuisha matumizi ya mitaro kuzuia mmomonyoko wa udongo na kuteka maji, matuta (terraces), zai pits (mashimo maalum kupanda mimea), inter cropping na cover cropping, na push and pull – matumizi ya mimea kama vile nyasi za mabingobingo (napier grass) na vitunguu kufurusha wadudu.
“Nyasi kama super Napier Pakchong, bhoma Rhodes na brachiaria ni faafu sana kufukuza wadudu waharibifu,” Rosemary anaelezea.
Huku matumizi ya dawa zenye kemikali kukabiliana na wadudu yakiwa kero kwa udongo na mazingira, mkulima huyu huchanganya na kupondaponda majani ya Sesbania na Gliricidia anayatumia.
Kando na kusifiwa kuangamiza wadudu, majani ya mmeahai huu (Sesbania) ni mbolea ya kijani na pia husaidia kudumisha hadhi ya udongo.
Maharagwe ya mucuna na soya, nayo huyalima kuongeza Nitrojini udongoni.
Mengine ni pamoja na Dolly Parton’s Cowboy Beans na jack – canavalia.
“Kwa sababu yanatambaa, huzuia kwekwe kukua,” Rosemary akaambia Akilimali wakati wa mahojiano shambani mwake Kijiji cha Shembekho.
Ana shamba la ekari mbili, ambalo anakiri tangu akumbatie matumizi ya teknolojia hizo za zamani kupitia hamasisho la SNV Netherlands Development Organisation, mwaka wa 2020, ameshuhudia mabadiliko makubwa kimapato.
SNV ni shirika la kimataifa lisilo la kiserikali (NGO), ambalo madhumuni yake ni kukabiliana na kero ya umaskini kupitia kilimo, na linaendeleza programu kadhaa za zaraa nchini Kenya.
Programu hizo zinapania kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi.
Rosemary alikuwa miongoni mwa wakulima walionufaika kupitia mpango wa Regenerative Agricultural practices for improved Livelihoods and Markets (REALMS), uliozinduliwa 2020 na kukamilika Oktoba mwaka huu, 2024.
“Mapato yameongezeka mara dufu na shamba langu kuwa na mpangilio,” mkulima huyo akasema.
Rosemary, kwenye mahojiano alisema amefunzwa haja ya kulima miti yenye thamani (agroforestry) hususan ya matunda na ile asilia kurejesha hadhi ya shamba na udongo.
SNV pia inaendeleza mpango wa kuhamasisha wakulima kukuza mboga za kienyeji.
Ni kupitia hamasisho la SNV kuanzia 2017 ilipotua Kakamega, Rosemary walifanikiwa kubuni Shembekho Self Help Group.
Kundi hilo lenye jumla ya wanachama 30; wanawake 21 na idadi iliyosalia ikiwa ni ya wanaume, liliundwa Machi 2020, na huongeza thamani mazao kwa kuyasindika.
Maharagwe ya mucuna, kwa mfano, huunda kinywaji sawa na chai, keki, unga wa kupika chapati na mandazi.
Soya nayo hutengeneza vitafunwa, kurina mafuta ya kupikia, na pia ni chakula cha mifugo.