Serikali kuanza kukata wananchi ada ya nyumba kwa mshahara
Na NICHOLAS KOMU
SERIKALI itaanza kuwatoza wafanyakazi wote wa umma na wa sekta ya kibinafsi asilimia 1.5 ya mshahara wao kufadhili mpango wake wa ujenzi wa makazi nafuu kuanzia Machi 1.
Waziri wa uchukuzi, makao na muundomsingi, James Macharia, Jumanne alisema ujenzi wa nyumba za bei nafuu utaendelea baada ya serikali kushauriana na vyama vya wafanyakazi na waajiri.
“Tulikuwa na maagizo ya korti ya kusimamisha mpango huu lakini pande zote zimekubaliana kuondoa kesi hizo na kwa hivyo tuko tayari kuendelea na mradi huu,” waziri Macharia alisema.
Hata hivyo, hakufafanua makubaliano kati ya serikali na Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (Cotu) ambao uliwasilisha kesi kusimamisha ada hiyo.
Bw Macharia alikuwa akizungumza akiwa Kaunti ya Nyeri alipokagua miradi ya serikali kuu. Aliahidi kumaliza soko la Chaka kufikia Aprili mwaka huu.
Jaji wa Mahakama ya Leba Hellen Wasilwa alitoa ilani ya kusimamisha serikali kutoza ada hiyo kufuatia ombi la Cotu.
Katika kesi iliyowasilishwa Desemba, Cotu ilisema utozaji wa ada hiyo ni kinyume cha sheria.
Katibu Mkuu wa Cotu, Bw Francis Atwoli alikosoa ada hizi ambazo serikali inasema zitahifadhiwa katika hazina ya kitaifa ya ustawi wa makao (NHDF). Bw Atwoli anasema pesa hizo zitaongezea wafanyakazi mzigo wa kulipa kodi.
Kulingana na Bw Macharia, ada hiyo itatozwa kuanzia Machi na kwamba utekelezaji wa mradi huo utaanza baada ya wiki chache.
“Mradi huo sasa uko wazi na utazindulia baada ya wiki chache. Nyumba za kwanza 2000 zitajengwa kwenye barabara ya Park Road, Nairobi,” alisema.
Alikariri kwamba wale ambao hawatafaidika na mradi huo watarudishiwa pesa zao baada ya kustaafu.
“ Wale ambao hawatapata nyumba au wale ambao wako na nyumba watarudishiwa pesa zao wakistaafu. Pesa ambazo hazitarudishwa ni za waajiri,” alisema.
Ada hiyo ya asilimia 1.5 kwa mishahara inatarajiwa kuleta takriban Sh57 bilioni kwa mwaka, kutoka kwa Wakenya karibu 2.5 milioni walioajiriwa, na kiasi zaidi kikitarajiwa kutoka kwa watu wanaochangia kwa hiari.
Ingawaje mpango wa awali ulikuwa kujenga nyumba nusu milioni, waziri alisema wajenzi wa humu nchini na kimataifa wameelezea nia ya kujenga nyumba milioni moja. Mradi huo unakisiwa kugharimu hadi Sh1.5 trilioni.