• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Walimu wanaosaka ajira wana hadi Februari 12 kutuma maombi

Walimu wanaosaka ajira wana hadi Februari 12 kutuma maombi

Na OUMA WANZALA

TUME ya Kuwaajiri walimu nchini (TSC) imetoa makataa ya hadi Februari 12 kwa walimu wanaosaka ajira kutuma barua zao za maombi za kuitaka kazi hiyo.

TSC inalenga kuwaajiri walimu 5,000 ili kusaidia kutekelezwa kwa mpango unaowataka wanafunzi wote waliofanya mtihani wa KCPE kujiunga na kidato cha kwanza ambao upo katika mwaka wake wa pili.

Afisa Mkuu Mtendaji wa TSC Nancy Macharia hata hivyo amesema kwamba wanaotuma maombi lazima wawe na umri usiozidi miaka 45 na pia lazima wawe wamesajiliwa na tume yake.

“Wanaotuma maombi ya kufundisha shule za upili lazima wawe na cheti cha stashahada au shahada katika kozi ya elimu na wanatakiwa kutuma maombi hayo kwa bodi simamizi za shule ambazo nafasi ya kazi ya ualimu imetangazwa kisha watume nakala ya maombi hayo kwa mkurugenzi wa TSC wa kaunti waliko,” akasema Bi Macharia huku akifichua kwamba tume yake inashughulikia suala hilo kupitia wakurugenzi wa kaunti na bodi za shule.

idadi ya walimu wanaoajiriwa itapandisha idadi ya jumla ya waliopokezwa kazi hiyo tangu mwaka jana hadi wa 12,000 na inatarajiwa kugharimu Sh3bilioni.

“Walimu hawa watasaidia kutekelezwa kwa sera inayosisitiza wanafunzi wote waliokamilisha darasa la nane wanajiunga na shule za upili,” akaongeza Bi Macharia.

Mwezi uliopita, TSC ilionya kwamba sekta ya elimu ingeathirika pakubwa iwapo walimu 70,000 hawangeajiriwa kusaidia kuimarisha mafunzo kwa idadi ya wanafunzi inayoongezeka shuleni kila mwaka.

TSC pia ilikuwa imependekezea serikali iwaajiri walimu 12,626 kila mwaka kwa kipindi cha miaka minne ijayo kuanzia mwaka jana, shughuli ambayo itaigharimu serikali Sh 8.3 bilioni kila mwaka.

Vyama vya KNUT na KUPPET vimekuwa katika mstari wa mbele kuishinikiza serikali kuwaajiri walimu zaidi ili wanafunzi waweze kupata elimu bora kinyume na sasa ambapo idadi ya walimu ni cha chini mno ikilinganishwa na wanafunzi.

You can share this post!

Raha kijijini chifu aliyetupwa jela miaka 11 kurejeshwa...

MOKUA: Mfumo wetu wa elimu wapaswa kusisitiza stadi za...

adminleo