Kumezwa kwa ANC na UDA presha kwa Weta, Kingi, Mutua kuvunja vyama
KUMEZWA kwa chama cha Amani National Congress (ANC) cha Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi na kile cha United Democratic Alliance (UDA) cha Rais William Ruto, kumewekea presha vyama vingine tanzu vya muungano wa Kenya Kwanza ambavyo vimekataa au kujivuta kuungana na chama hicho tawala.
Rais William Ruto amekuwa akisisitiza kuwa vyama tanzu 18 vya muungano wa Kenya Kenya vinapaswa kuvunjwa ili kuunda chama kimoja chenye nguvu, wito ambao umekuwa ukipingwa na baadhi ya vyama hivyo.
Mnamo Ijumaa, UDA na (ANC) vilikamilisha mchakato wa kuungana na kutangaza kuundwa kwa chama cha United Democratic Alliance Party ambacho kitakuwa na alama na rangi zinazoakisi vyama hivyo viwili.
Mwenyekiti wa UDAP, Cecily Mbarire alisema hatua hii ilijiri baada ya miezi kadhaa ya mazungumzo. ANC ni chama tanzu cha muungano tawala wa Kenya Kwanza.
Issa Timami aliyekuwa mwenyekiti wa ANC, atakuwa naibu kiongozi wa chama kipya. Makamu Mwenyekiti wa chama hicho atakuwa Kelvin Lunani, huku Naibu Katibu Mkuu akiwa Omboko Milemba.
Kulingana na Mbarire, shughuli ya kuunganisha vyama hivyo viwili ilianza mapema mwaka jana lakini ikalazimika kukwama kufuatia changamoto zilizokuwa zikikabili chama tawala.
Wadadisi wa siasa wanasema hatua hiyo itaongeza presha kwa vyama vingine vikuu vya muungano huo hasa vile ambavyo vinara wao wamepatiwa kazi na serikali au walipata nyadhifa kufuatia ushirikiano wao na UDA.
Wanasema wanaolengwa kwa shinikizo hizi ni Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula ambaye chama chake cha Ford Kenya kimekuwa kikijivuta kumezwa na UDA na mwenzake wa Seneti Amason Kingi aliyeongoza chama cha Pan African Alliance (PAA) kujiunga na Kenya Kwanza.
Wengine ni Alfred Mutua wa chama cha Maendeleo Chap Chap ambaye ni waziri wa Leba na mwenzake wa Utumishi wa Umma Justin Muturi anayehusishwa na chama cha Democratic Party na Mwangi Kiunjuri wa chama cha The Service Party.
Vyama vingine vya muungano wa Kenya Kwanza ni Chama cha Mashinani ambacho kinahusishwa na aliyekuwa gavana wa Bomet Isaac Rutto anayehudumu katika Tume ya Huduma ya Mahakama, Tujibebe Wakenya Party ambacho kiongozi wake William Kabogo aliteuliwa waziri wa ICT na Uchumi Dijitali.
Farmers Party cha aliyekuwa katibu wa wizara Irungu Nyakera na United Democratic Movement kinachohusishwa na seneta wa Mandera Ali Roba miongoni mwa vingine.
Mwaka jana, wakati ANC ilipotangaza ilikuwa ikizungumza na UDA kuelekea muungano ambao ulikamilika jana, Katibu Mkuu wa Ford Kenya John Chikati alisema chama hicho chenye alama ya simba hakitavunjwa.
“Kumekuwa na uvumi kwamba vyama vinavunjwa. Kwanza, hakuna mtu aliyekuja kwetu kutuomba tuvunje chama chetu. Hata kama wangetuuliza, Ford Kenya hawawezi kuvunjwa,” alisema Chikati, baada ya mkutano wa kamati simamizi ya chama mwaka jana.
Aliongeza: “Tutaendelea kuwepo. Baadhi ya vyama ibuka vitaondoka na kuacha Ford Kenya uwanjani. Hatutavunja chama, tunaweza tu kukipanua na kuacha chama hiki kwa kizazi kijacho.”
Mchambuzi wa siasa Edna Musili anasema kumezwa kwa ANC ni mkakati wa kisiasa unaolenga kushinikiza vyama tanzu vya Kenya Kwanza kuvunjwa anavyotaka Rais Ruto japo kiongozi wa nchi awali alisisitiza hakuna chama kitakacholazimishwa kuvunjwa.
“Kuna presha kubwa kwa vyama tanzu vya Kenya Kwanza kuvunjwa na hatua ya ANC ilikuwa ya kutuma ujumbe kwa vinavyojivuta kuungana. Kumbuka Rais ana washirika wapya na wenye nguvu kama Orange Democratic Movement (ODM) na anaweza kusema hahitaji washirika wake katika Kenya Kwanza,” asema Bi Musili.
Katika siasa, asema mdadisi wa siasa Dkt Isaac Gichuki, mambo hayafanyiki bila malengo yaliyokusudiwa na kumezwa kwa ANC na UDA ni mkakati wa kuvua vyama vinavyojivuta kukubali wito wa rais anapojiandaa kugombea muhula wa pili.
“Kuna uwezekano mkubwa kwamba vyama vingine vitafuata mkondo wa ANC na vile ambavyo havitafanya hivyo vitalaumiwa kwa kuyumbisha ajenda ya rais na vitisho vitaanikiza katika mikutano ya hadhara kutoka kwa wakereketwa wa UDA,” akasema.