Akili MaliMakala

Sababu za wafugaji kujiundia malisho

Na SAMMY WAWERU January 20th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

KWA muda wa miaka minne mfululizo, wafugaji nchini wamekuwa wakilalamikia gharama ya juu ya chakula cha mifugo.

Mfumko huo wa bei, ulianza kushuhudiwa mwaka wa 2020 Kenya ilipothibitisha kuwa mwenyeji wa ugonjwa wa Covid-19.

Janga hilo la kimataifa, hata hivyo, miaka miwili baadaye Shirika la Afya duniani (WHO) lilitangaza ulimwengu kuwa huru.

Kenya huagiza kutoka nje zaidi ya asilimia 80 ya malighafi yanayotumika kuunda malisho ya mifugo, na mlipuko wa virusi vya corona ambao ulisambaratisha biashara nyingi uliathiri upatikanaji wake.

Mbali na malighafi kuadimika, serikali inanyooshewa kidole cha lawama kuyatoza ushuru wa juu hivyo basi kuchochea chakula cha wanyama kuwa ghali.

Mfugaji wa kuku Kiambu, Teresiah Gathii akionyesha chakula alichounda. PICHA|SAMMY WAWERU

Licha ya changamoto hizo, wakulima wamefunguka macho na kuanza kujitengenezea malisho.

Teresiah Gathii, ni mmoja wa wafugaji ambao wanatekeleza shughuli hiyo.

Hufuga kuku wa mayai katika Kaunti ya Kiambu.

“Kwa kujitengenezea chakula, nimefanikiwa kupunguza gharama ya uzalishaji kwa karibu asilimia 50,” anasema.

Mama huyu aliyeingilia biashara ya ufugaji wa kuku zaidi ya miaka 12 iliyopita, ana mashine ya shughuli hiyo – kisiagi.

Anadokeza kwamba hununua malighafi yakiwemo madini faafu kwa kuku, na kujiundia malisho.

“Nina fomula ya kutengeneza chakula cha kuku ninayofuata,” Teresiah anaelezea.

Kelvin Kilonzo ni mfugaji mwingine wa kuku anayejiundia malisho.

Kelvin Kilonzo akilisha kuku wake. PICHA|SAMMY WAWERU

Kulingana na Kilonzo, ni nafuu kujitengenezea chakula cha mifugo kuliko kutegemea kile cha madukani ambacho ni ghali.

“Baadhi ya vyakula vya madukani havijaafikia ubora wa bidhaa,” Kilonzo anasema.

Kilonzo anaendeleza ufugaji wa kuku wa mayai na nyama katika Kaunti ya Kiambu na Machakos.

Kwa wafugaji wa mifugo kama vile ng’ombe, nao wanalima nyasi kisha wanawapa wanyama wao.

“Ninapunguza gharama ya chakula kwa kulima nyasi maalum aina ya Juncao,” anasema Sammy Kariuki, mfugaji wa ng’ombe wa maziwa Nakuru.

Ng’ombe wa Sammy Kariuki, mfugaji Nakuru wakila nyasi maalum aina ya Juncao. PICHA|SAMMY WAWERU

Juncao ni nyasi yenye asili ya China, na yenye virutubisho tele.

Nyasi zingine zinazoshabikiwa na wakulima ni Pakchong Super Napier.