Kimataifa

Trump atumia mamlaka yake kusamehe wafuasi 1,500 waliovamia jengo la Bunge 2021

Na MASHIRIKA January 21st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WASHINGTON, AMERIKA

RAIS Donald Trump alianza uongozi kwa kutekeleza mabadiliko mengi ya sera Amerika baada ya kuapishwa mnamo Jumatatu usiku.

Hata kabla wino kukauka, Rais Trump alitia saini amri ambazo zitadhibiti uhamiaji haramu, kuondoa baadhi ya sheria za mazingira, jinsia na rangi.

Jana, Trump alitumia mamlaka yake kuwasamehe wafuasi wake 1,500 ambao walivamia jengo la Capitol miaka minne iliyopita. Wafuasi hao walikuwa wakiandamana mnamo Januari 6, 2021 wakidai Rais Trump alishindwa na aliyekuwa Rais kwa njia isiyofaa kwenye uchaguzi huo wa 2020.

Hatua yake inafasiriwa kama itakayowakasirisha polisi, wabunge miongoni mwa watu wengine ambao walizima maandamano hayo yaliyotishia kupaka tope sifa za Amerika ulimwenguni.

Polisi 140 waliumia kwa kupigwa wakati wa maandamano hayo, baadhi wakinyunyuziwa kemikali hatari, wakapigwa na mabomba ya maji, miti na silaha nyingine hatari.

Watu wanne waliaga dunia akiwemo mfuasi wa rais huyo aliyepigwa risasi.

Akihutubu wakati wa kuapishwa kwake, Trump alijisawiri kama kiongozi ambaye alichaguliwa kupitia uwezo wa mwenyezi Mungu.

Kauli yake ilionekana kurejelea matukio mawili ambapo alinusurika kifo baada ya kulengwa kwa risasi wakati wa kampeni za uchaguzi wa Novemba mwaka jana.

“Niliokolewa na Mungu ili nifanye Amerika iwe bora tena,” akasema.

Trump ni rais wa kwanza kwa zaidi ya miaka 100 kushinda muhula wa pili baada ya kuhudumu muhula wa kwanza kisha kupoteza urais.

Pia ni rais mkongwe zaidi kuwahi kuapisha Ikulu ya White House na pia rais wa kwanza aliyehukumiwa kufungwa kuhudumu kama kiongozi wa Amerika.

Baada ya kuapishwa, alitekeleza ahadi yake ya kuzima wahamiaji haramu. Utawala wake jana uliondoa mpango ambao uliruhusu maelfu ya wahamiaji kuingia Amerika huku mipango iliyokuwa ikiendelea ikizimwa.

Kati ya walioathirika walikuwa zaidi ya raia 1,600 wa Afghanistan ambao walikuwa wamepewa kibali na serikali ya Joe Biden ili waishi Amerika.

Akiwa Ikulu ya White House, Rais Trump alitia saini amri ya kuwaweka wanajeshi kwenye mpaka wa Amerika na Mexico kuwazuia wahamiaji, walanguzi wa dawa za kulevya na wale aliowarejelea kama makundi ya kigaidi kutoka Mexico.

Pia alitia saini amri inayozuia wale ambao wamezaliwa Amerika na ni raia wa kigeni, kupata uraia wa nchi hiyo yenye uchumi mkubwa duniani.

Hakukomea hapo kwa kuwa aliondoa Amerika kutoka kwenye mkataba wa tabianchi ya Paris, hatua ambayo itadidimiza juhudi za kupambana na juhudi za kupambana na uchafuzi wa mazingira.

“Tunaondoa saratani yote ambayo Amerika imeletwa na utawala wa Rais Biden,” akasema.

Pia alitoa amri za utawala wa Biden zilizoongoza teknolojia ya akiliunde na magari yanayotumia umeme. Wakati wa utawala hakuna mfanyakazi atawajibika akiwa nyumbani akiwaamrisha wote warejee afisini na kuwahudumia raia.

Amerika ambayo imekuwa ikitoa ufadhili mkubwa zaidi kwa Shirika la Afya Duniani (WHO) haitafanya hivyo tena.

Rais Trump aliondoa nchi kwenye shirika hilo akisema limekuwa likinyonya Amerika hela ambazo zinastahili zitumike kujenga nchi hiyo.

Pia makundi ya mashoga sasa ni haramu Amerika, Trump akisema utawala wake unatambua jinsia ya kike na kiume pekee, hatua ambayo imelaaniwa na mashirika ya haki.