• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 12:48 PM
Hoteli za kifahari Pwani zapiga marufuku chupa za plastiki

Hoteli za kifahari Pwani zapiga marufuku chupa za plastiki

Na WINNIE ATIENO

HOTELI za kifahari katika ufuo wa Pwani zimepiga marufuku utumizi wa mirija na chupa za maji za plastiki kutumika katika mikahawa ya kitalii huku vita dhidi ya matumizi ya plastiki vikishika kasi nchini.

Chupa za plastiki zimetajwa kuchangia uchafuzi wa mazingira hasa katika maji ya Bahari Hindi na kuathiri maisha ya samaki.

Hoteli hizo za Serena, Diani Reef, Sarova Whitesands, Tamarind Mombasa, Sands huko kisiwani Chale na ile ya ufuoni ya Swahili zimeapa kukabiliana na matumizi ya plastiki katika mikahawa ya kifahari.

Hoteli nyingine ni Lantana Galu, Baobab, Afro Chic Diani, Medina Palms, Turtle Bay, Severin Sea Lodge, Kenya Bay.

Wageni na watalii watakaozuru mikahawa hiyo watapewa maji kwa chupa za glasi na metali kama njia moja ya kuhifadhi mazingira.

Kwenye kampeni hiyo ya Umoja wa Mataifa na shirika la utalii nchini linaloendeleza uhifahdi wa mazingira, wawekezaji hao wananuia kuhakikisha eneo la Pwani inasalia bila plastiki.

“Tunawapa wageni wetu na watalii maji ya kunywa kwa glasi ama chupa maalum ambayo si plastiki. Kando na hilo, tunawahamasisha wafanyakazi wetu kuhusu uhifadhi wa mazingira,” Bw Mwahunga alisema.

Katika hoteli ya ufuoni ya Serena, Mombasa, meneja mkurugenzi Bw Tuva Mwahunga alisema mkahawa huo umeanza mikakati ya kukabiliana na plastiki.

“Hoteli ya Serena inatumia teknolojia kukabiliana na uchafuzi wa mazingira. Wakenya wanafaa kuhifadhi mazingira,” Bw Mwahunga alisisitiza akiongeza kuwa Wakenya wana uzoefu wa kutumia plastiki ilhali ina madhara yake.

“Hususan kwa samaki, ndege wa angani, na wanyama wetu wa pori. Pia plastiki zinaathiri bahari,” aliongeza.

Katika hoteli ya Diani Reef meneja mkurugenzi Bw Bobby Kamani alisema mirifa ya plastiki haitumiki tena.

“Sasa tunatumia mirifa yakutengenezwa na bamboo. Pia tuko mbioni kukabiliana na matumizi ya chumba za plastiki, ” Bw Kamani aliiambia Taifa Leo.

Agosti 29 mwaka wa 2017, serikali ilipiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki hata hivyo changamoto kufuatia agizo hilo bado imekithiri.

Kulingana na katibu mkuu wa Mazingira na Misitu Ali Noor Ismael vyombo vya serikali husika ikiwemo serikali ya kaunti inafaa kukaza Kamba na kuhakikisha matumizi ya mifuko ya plastiki yanakomeshwa.

You can share this post!

Jaji akosoa jamii kwa kusamehe wabakaji badala ya kuwashtaki

SOLAI: Makabiliano ya polisi na wakazi wanaotaka fidia...

adminleo