Jamvi La Siasa

Jinsi mzozo DRC unaweza kuathiri nafasi ya Raila kushinda kiti cha AUC Februari 15

Na JUSTUS OCHIENG, CHARLES WASONGA January 31st, 2025 Kusoma ni dakika: 3

RAIS William Ruto anakumbwa na kibarua kigumu kama mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) katika mazungumzo ya amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) huku wataalamu wakionya kuwa huenda maamuzi yao kuhusu suala hilo yakaathiri nafasi ya Raila Odinga kushinda uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).

Huku uchaguzi wa AUC, ulioratibiwa kufanyika Februari 15, mwaka huu, ukikaribia, Dkt Ruto anakabiliwa na kibarua cha kurejesha amani DRC kabla ya siku hiyo.

Hii ni kwa sababu kuna hofu kwamba mzozo nchini DRC tayari umeibua taharuki ambayo huenda ikaathiri jinsi marais wa mataifa wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Afrika Kusini (SADC) na EAC watapiga kura Februari 15.

Wataalamu wanasema ushindi wa Bw Odinga utategemea pakubwa na jinsi Rais Ruto, kama mwenyekiti wa EAC, atakavyoshughulikia changamoto hizi za kidiplomasia kabla ya uchaguzi.

Tayari mazungumzo ya amani yanayoongozwa na Ruto yalianza vibaya Jumatano, Januari 29 baada ya Rais wa DRC Felix Tshisekedi kususia kikao cha kujadili kuzorota kwa usalama Mashariki mwa nchi hiyo.

Hata hivyo, Tshisekedi alithibitisha kuwa angehudhuria mkutano wa kuhusu suala hilo ulioitishwa na jumuiya ya SADC jijini Harare, Zimbabwe Alhamisi, Januari 30, 2025. Mkutano huo uliongozwa na Rais wa nchi hiyo Emmerson Mnangagwa.

Hali hii imeonekana kutilia shaka kujitolea kwa Tshisekedi kwa masuala ya jumuiya ya EAC na kutothamini mazungumzo yanayoongozwa na Rais Ruto.

Hatua ya Rais huyo wa DRC kukwepa mkutano wa ulioitishwa na Ruto inathibitisha imani ya kiongozi huyo, na raia wa nchi yake, kwamba Kenya inaunga mkono Rais wa Rwanda Paul Kagame. Bw Kagame anatuhumiwa kuunga mkono, na kufadhili, waasi wa M23, tuhuma ambazo amekana vikali, mara si moja.

Kando na mkutano wa SADC wa Alhamisi, Januari 30, Jumanne, Januari 28 Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan aliongoza mkutano mwingine wa marais wa mataifa ya Afrika Kusini, yakiwemo yale yaliyochangia wanajeshi katika kikosi cha SADC kilichoko DRC (SAMIDRC).

Rais Samia ni mwenyekiti wa Asasi ya SADC kuhusu Siasa, Ulinzi na Ushirikiano wa Kiusalama japo Tanzania pia ni mwanachama wa EAC.

SADC inashirikisha mataifa 16 wanachama wenye uwezo wa kuyumbisha uchaguzi wa AUC endapo yatahisi kuwa Kenya ni kikwazo katika usuluhishaji wa mzozo nchini DRC.

Jumuiya za kikanda zinaendeleza juhudi za kusaka njia za kukomesha mapigano katika mji mkuu Mashariki wa DRC, Goma na taharuki katika jiji kuu Kinshasa.

Kufikia Alhamisi jioni, zaidi ya watu 100 walikuwa wameuawa na wengine 3,000 kujeruhiwa tangu wapiganaji wa M23 walipoingia Goma Jumapili usiku na kuanza kukabiliana na wanajeshi wa serikali wanaosaidiwa na kikosi cha SAMIDRC.

“Kutekwa kwa Goma, ambako kungezuiwa na EAC, kunazipa nchi jirani kisingizio cha kuielekezea Kenya kidole cha lawama. Mchakato wa awali wa kuleta amani ulishirikishwa kutoka Nairobi chini ya usimamizi wa Rais mstaafu Uhuru Kenya na uenyekiti wa sasa wa EAC ni wetu,” anasema balozi wa zamani wa Kenya nchini Korea Ngovi Kitau.

Anaongeza: “Kenya haijakuwa ikudumisha mahusiano na majirani kwa kipindi kirefu. Hii ndio maana tulipoteza kiti cha AUC kwa Chad (ambayo raia wake Moussa Faki ndiye mwenyekiti wa sasa wa AUC) mnamo 2017.

Bw Kitau anasema kuwa hata nchi zingine jirani hazikuunga mkono mgombeaji wa Kenya wakati huo waziri wa zamani Amina Mohamed akisema “uadui huu unapasa kushughulikiwa kwa dharura”.

Kwa upande wake Profesa Peter Kagwanja anasema kutekwa kwa Goma, mji mkuu wa mkoa wa Kivu Kaskazini, na waasi wa M23 kumeitumbukiza EAC katika mzozo mbaya zaidi.

“Kufeli kwa Kenya kuhakikisha makundi hasimu yanasitisha vita ili kuzuia kutokea kwa changamoto ya kibinadamu huenda kukaigharimu Kenya katika uchaguzi wa AUC utaofanyika baada ya majuma matatu yajayo,” anaeleza Profesa Kagwanja ambaye ni mtaalamu wa masuala ya uongozi, usalama na masuala ya Afrika.

Msomi huyo, ambaye ni Afisa Mkuu Mtendaji wa Shirika la kuchambua Sera barani Afrika, anaongeza kuwa kufeli kupatikana kwa suluhu la kudumu kwa mzozo wa DRC kunaboronga sifa za Kenya katika nyanja ya kidiplomasia.

“Aidha, hali hiyo inatilia shaka uwezo wa asasi ya jumuiya ya EAC ya kusuluhisha mizozo.”

Naibu Gavana wa Machakos Francis Mwangangi, ambaye ni mtaalamu wa masuala ya mahusiano ya kimataifa anasema jinsi Kenya itakavyoshughulikia mzozo wa DRC ama kutafaidi au kuathiri ndoto za Odinga za kutwaa wadhifa wa AUC.

“Endapo viongozi wa nchi wanachama wa AU watahisi kuwa Kenya sio mpatanishi mzuri, hali hii itaathiri nafasi ya Bw Odinga kutwaa kiti hicho. Lakini marais na viongozi wa nchini wakishawishika kuwa Kenya inachangia pakubwa na inajaribu kushughulikia mzozo huo kwa njia nzuri, basi hiyo itamsaidia Odinga,” Bw Mwangangi anasema.

Bw Odinga ambaye ni waziri mkuu wa zamani wa Kenya anamenyana na wagombeaji wawili; Mahmoud Ali Youssouf na Richard Randriamandrato wa Madagascar.