Ya Rabi inusuru Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
KWA jina la Mwenyezi Mungu mwenye kuneemesha neema kubwa kubwa na neema ndogo ndogo. Kwa kudura zake Muumba wetu asiyefananishwa na chochote, tumejaaliwa tena kuonana leo ili kukumbushana neno lake.
Allah (SWT) pekee anayestahili kuabudiwa na kuenziwa kwa hali zote, Muumba wa ardhi na mbingu na vyote vilivyomo. Baada ya kumpwekesha Mola wetu tunachukua uzito wa nafasi hii kumtilia dua mwombezi wetu Mtume (SAW). Leo hii ndugu zangu waumini wa dini hii tukufu ya Kiislamu tunakutana huku dunia ikiwa imejawa na vurumai kila kona. Ya Rabi twakulilia nusra yako, hakuna tena amani katika ardhi yako. Hadi lini?
Katika ukumbi wetu huu kila leo, kila nukta, tumekuwa siku zote tukimuomba Muumba wetu kuwe na amani na utulivu katika ardhi yake hii. Alhamdulillahi. Hali imeanza kutulia nchini Lebanon. Aidha, kuna amani na tabasamu angalau huko Palestina ingawa nchi hiyo ni magofu matupu. Israel imeiacha ardhi ya Gaza ikiwa ombwe tupu. Wanarudi nyumbani Wapalestina lakini si kama nyumbani tena. Pawe nafuu huko Gaza.
Vipi hali katika pembe nyinginezo za dunia? Hali ni taaban!
Sasa hivi hali ni tete mno katika taifa la Sudan hadi kwa jirani wake Sudan Kusini. Ugumu wa hali ya maisha kutokana na mapigano Sudan umesababisha mitandao kufungwa. Ya Allah!
Katika nchi ya Ukraine hali ingali kama juzi na jana. Viongozi wakuu duniani wanapiga domo na kukutana katika mahoteli wakizidisha vikwazo, lakini Urusi ingali inaangusha makombora na silaha kali kali dhidi ya jirani yake Ukraine.
Juzi nimekwenda kinyozi na kisadfa nikapata kinyozi mmoja ni ndugu yangu kutoka katika Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC). Kilikuwa ni kilio kitupu. Kila tukitazama runinga na ndugu yangu huyo, machozi yalitutiririka. Ni miaka kumi tangu amekimbia nchini mwao kutokana na ghasia. Hadi leo hali ingali ngumu.
Mpaka wa DR Congo na Rwanda umefungwa. Balozi za nchi kadha zimeshambuliwa. Viongozi wa kanda nao wanalumbana. Kundi la waasi la M23 na jeshi la DRC ni mateke na silaha tupu. Wanawake, watoto, wanaume ni mbio na roho mkononi.
Ewe Mola wetu, leta suluhu nchini DR Congo In Shaa Allah.