SACHANGWAN: Uchungu miaka 10 baada ya Wakenya 199 kuangamia kwa moto
Na PETER MBURU
UNAPOMWONA akiwa katika pilkapilka za kufanya kazi za sulubu, huenda ukahadaika kuamini kuwa ni kijana tu kama wengine chipukizi uwajuao, walio imara kiafya.
Lakini mawazoni mwa Nicholas Kipchirchir, 23, kuna mengi yaliyofichika na historia pevu iliyojikita ndani ya umri mdogo.
Mnamo 2009, alipokuwa na miaka 13, Jumamosi moja tulivu walipokuwa wakicheza soka na watoto wenzake, tukio moja lilitendeka ambalo lilibadili mkondo wa maisha yake.
Walisikia mlio wa ajabu ghafla, kisha ukemi wa muda. Baadaye, walifahamishwa kuwa lori la mafuta lilikuwa limepata ajali, na kuwa watu walikuwa wakikimbia eneo lile, Sachangwan-kando ya barabara, kuchota mafuta.
Hapo, zaidi ya watoto 22, wachezaji na mashabiki walitoka mbio kuelekea eneo hilo.
“Tulipofika, kukaa kidogo tu nikaona moto, hata sikuwa nimeanza kuchota, nilikuwa nikitafuta kitu cha kutmia kubeba. Kutaka kukimbia nilianguka ndani ya mtaro uliokuwa karibu na muda si muda moto ukanifunika,” Nicholas anaeleza.
Matokeo yake yalikuwa kijana huyo kuungua vibaya miguuni, mikononi, kichwani, usoni na sehemu za kiuno na mgongo.
Alilazwa hospitalini akiwa katika hali mbaya kwa wiki mbili, kisha baada ya kuruhusiwa kwenda nyumbani akaendelea kupata matibabu katika kifaa cha afya ndani ya kambi ya GSU iliyoko karibu na nyumbani kwao.
“Kati ya watoto tulioenda nao, wawili walikufa motoni na wengine wakaungua vibaya,” akasema Nicholas, ambaye ni yatima. Hadi sasa anaishi kwa jirani yao aliyechukua jukumu la kumlea.
Na japo uchungu wa vidonda ulimwisha, kila anapoona alama alizoachiwa maeneo ya mwili alipoungua huwa anakumbuka siku hiyo ambayo alikumbana ana kwa ana na kifo. Ni jambo ambalo bado linamtatiza, miaka kumi baadaye.
Kilomita chache kutoka nyumbani kwa Nicholas, jamaa mwingine (ambaye anakataa kutambulishwa) ambaye pia aliungua katika mkasa huo naye anaendelea na maisha yake, akifanya kazi ya kuchoma makaa eneo hilo la Sachangwan.
Hata hivyo, kila anapofanya kazi yake hiyo, kuona moto humkumbusha hatari aliyokumbana nayo miaka kumi mbeleni. Anapofunua mguu na kuona alama aliyoachiwa na moto huo, damu humkimbia na kutamani kuwa maisha yangekuwa afadhali, asilazimike kuona moto kila siku ya maisha yake.
Hata hivyo, kunao baadhi yao ambao licha ya kuadhirika na moto huo walijikakamua na kujiinua, wengine wakifanya kazi na wengine kuendeleza masomo na sasa wamebadili maisha.
Mmoja ni kijana mhudumu wa afya eneo la Wajir (ambaye pia hakutaka kutambulishwa kutokana na hali kuwa ni mtumishi wa umma aliyeajiriwa majuzi), ambaye licha ya kuungua vibaya na maisha yake kuhatarishwa wakati moto huo ulipotokea, baadaye alijinyanyua tena na kuendeleza masomo hadi chuoni.
Bali na walioadhirika moja kwa moja, familia za watu waliofariki katika mkasa huo ndizo ziliachwa na makovu mabaya ya rohoni, kwani wengine hadi leo hawajawahi kupona na kwa wengine hali hiyo iliishia kuadhiri jamaa zao kiafya na kisaikolojia.
Kwa baadhi ya watu, ndugu, wazazi ama watoto wa walioaga walipopata habari walishtuka na kupata magonjwa mbalimbali ama wengine hata kupata ajali ambazo zinawaadhiri hadi leo.
Katika kituo cha kibiashara cha Sachangwan, kilomita kadha tu kutoka ambapo mkasa huo wa moto ulitendeka, Bi Cecilia Wambui anaketi katika kiti moto, akichoma mahindi ya kuuza, kando na kibanda chake cha kuuza vyakula na viungo vya upishi.
Kando yake, ameketi kijana wake wa kiume, Peter Kimani ambaye hawezi kujifanyia lolote. Anafanyiwa kila kitu kama mtoto kutokana na ugonjwa aliopata miaka kumi iliyopita.
“Aliposikia kuwa ndugu yake amefariki baada ya mkasa wa moto 2009, alishtuka sana na tangu wakati huo amekuwa mgonjwa, hajawahi kupona. Huwa tunakaa naye nikimchunga kama mtoto tu,” Bi Wambui anasema.
Anakumbuka vyema namna mkasa huo ulimpokonya mwanawe kifungua mimba, Alex Mwaura, ambaye alikuwa makanika katika mtaa huo. Mama huyo alitarajia kuwa marehemu ndiye angekuwa tegemeo la familia baada ya kumpeleka chuo kusomea kozi hiyo, alipokosa karo ya shule ya upili.
“Haya ni mawimbi ambayo ni kama yalikuja kuwinda vifungua mimba na watu waliokuwa tegemeo la familia zao tu,” anasema mama huyo, wakati wote huu mawazo yake yakivurugika kwa kukumbushwa kitu ambacho huchoma moyo wake.
Hali si tofauti kwa Bi Anne Kebenei, mama ambaye anafahamu fika kiwango cha hasara ambacho mkasa huo uliacha.
Mbali na kuwapoteza mume na mwanawe wa kiume wakati huo, mwaka uliopita aidha mwanawe mwingine aligongwa na gari na kufa eneo hilo, karibu na kaburi walipozikwa waliokufa.
Mvulana huyo alikuwa akiuza miwa katika barabara hiyo ili kujipatia riziki na Bi Kebenei anaamini kuwa hali ya mumewe ambaye alikuwa tegemeo la familia kufa kwenye mkasa ndiyo iliwasukuma pamoja na wanawe kujituma kutafuta riziki na baadaye kusababisha mkasa mwingine.
Familia zaidi za waathiriwa hao zinalia kuwa zimekuwa zikiishi bila usaidizi na kulaumu kuwa serikali iliwatelekeza, licha ya matatizo mengi waliyoachiwa na hali kuwa viongozi wa kisiasa wamekuwa wakitumia mkasa huo kujipigia debe wachaguliwe, japo wanapoingia maofisini wanawasahau.
“Viongozi wakati wa kampeni huja na kutumia suala hili kusema kuwa watatutetea lakini baada ya kuchaguliwa hatuoni kitu. Watoto ni wengi tuliwachiwa, na wajane wengi sasa wako na kilio kabisa. Wale waliungua, wengine wamekufa na wengine bado wako,” Bi Rose Koech ambaye naye alimpoteza mwanawe kwenye mkasa huo anasema.
Anaendelea kuwa hawajakata tamaa, akisema “Tunaomba tu usaidizi, hatujakufa moyo, kwa sababu ile shida tulipata tungali tunabebana nayo matumboni mwetu hadi leo.”
Katika kaburi hilo la umma, mabaki ya watu 78 ambao waliungua kabisa kiwango cha kutojulikana yamelazwa, huku majina ya watu 130 kwa jumla ambao waliungua vibaya (wengine wakiwa walizikwa na familia zao) yakiorodheshwa.
Watu wengine 69 walikufia mahospitalini, wakifanya idadi jumla ya waliokufa wakati huo 199. Hata hivyo, jinsi muda umekuwa ukisonga, waadhiriwa wengine wamepoteza maisha na sasa idadi kamili haiwezi kujulikana.
Ni katika kaburi hilo ambapo jamaa na familia huja mwaka baada ya mwingine kujiliwaza wanaposoma majina ya wapendwa wao, na huenda wanahisi utulivu wa rohoni.
Na si familia tu, kwani watu wa matabaka mbali mbali hutoka kila kona ya Kenya hufika eneo hilo kushuhudia athari za mkasa huo.
Waathiriwa wanadai kuwa serikali ya Rais Mustaafu Mwai Kibaki iliwaahidi fidia ya Sh30 milioni japo hawajawahi kuziona, nao maafisa wa serikali wakisema hawafahamu kitu kama hicho.
“Nilikuwa nikifuatilia mambo haya hadi katika ofisi ya mkuu wa mkoa, mambo yakaenda hadi kufikia ofisi ya Rais Kibaki. Kibaki akasema atatupea Sh30 milioni nilipokuwa ikulu. Tulijaribu kuzifuata lakini ukawa ni msemo tu alisema,” Bi Koech akasema.
Chifu wa eneo hilo Evans Mageto, hata hivyo, alisema ofisi yake haikupata ripoti hizo, japo akikiri kuwa waathiriwa bado wana matatizo mengi ambayo yanahitaji mkono wa serikali ama wasamaria wema.
“Suala la fidia ya Sh30 milioni hatukulisikia na ikiwa lipo linaweza kufatiliwa. Lakini kuna watu ambao hadi sasa bado wanahitaji kusaidiwa kwa njia moja ama nyingine. Kunao walio na uchungu mwingi,” Bw Mageto akasema.
Ni matamshi ambayo diwani maalum kutoka eneo hilo Rachael Maru alikariri, akisema kuwa walioathiriwa wanaishi na shida nyingi.
“Wajane hawana uwezo kwa kuwa wanateseka kupata lishe na karo, nao vijana walioungua hawawezi kusimama kwa muda mrefu na hivyo wakitafuta kazi hawapati,” akasema Bi Maru.
Ni miaka kumi sasa tangu kisa hicho, na japo huenda mkasa wenyewe ulisahaulika na wengi wa Wakenya, ni bayana kuwa kwa mamia ya familia ambazo ziliathirika, juhudi za kusonga mbele kimaisha zimekuwa zikumbwa na kizingiti cha mkasa huo.