Uteuzi wampa Jumwa nguvu mpya kisiasa
HATUA ya Rais William Ruto, kumwajiri aliyekuwa Waziri wa Jinsia, Bi Aisha Jumwa, serikalini imeibua msisimko mpya wa kisiasa kuhusu uchaguzi ujao katika Kaunti ya Kilifi.
Kabla kuteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Barabara nchini wiki chache zilizopita, Bi Jumwa alikuwa mpweke kisiasa.
Alitumia muda wake mwingi kufanya mikutano mashinani Kilifi, huku akionekana kuweka misingi ya kinyang’anyiro cha ugavana 2027.
Katika kipindi hicho, msimamo wake wa kisiasa haukuwa wazi baada ya kukosa teuzi kadha za kazi serikalini huku ripoti zikienea kwamba anawazia kujiondoa katika chama cha UDA, ingawa aliendelea kusisitiza uaminifu wake kwa Rais.
Hata hivyo, mambo sasa yanaonekana kubadilika kama ilivyoshuhudiwa wakati wa hafla yake ya shukrani iliyofanyika Malindi wikendi.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na vigogo wa kisiasa wa Pwani wakiongozwa na Waziri wa Madini, Uchumi wa Baharini na Ubaharia, Bw Hassan Joho, Katibu Mkuu wa Chama cha UDA, Bw Hassan Omar, na Naibu Kiongozi wa chama hicho, Bw Issa Timamy.
Ikumbukwe kwamba Bi Jumwa hakuwahi kufanya hafla yoyote aina hiyo wakati alipoteuliwa kwa mara ya kwanza kuwa Waziri wa Utumishi wa Umma na baadaye akawa Waziri wa Jinsia.
Hafla hiyo ya Jumapili katika Uwanja wa Msabaha ulio katika ngome yake ya kisiasa Kaunti Ndogo ya Malindi, pia ilihudhuriwa na Waziri wa Michezo, Bw Salim Mvurya na wabunge mbalimbali kutoka ukanda wa Pwani.
Hata hivyo, wanasiasa wengi wa Kilifi wakiongozwa na Gavana Gideon Mung’aro ambaye ni wa chama cha ODM na wabunge wa eneo hilo, walisusia.
Wazungumzaji kadha kwenye hafla hiyo waliapa kumuunga mkono katika azma yake ya kumvua madaraka Bw Mung’aro mnamo 2027.
Bw Omar aliwakemea wanachama ambao wamekuwa wakiwatishia wafuasi wa Bi Jumwa.
“Hakuna mtu katika UDA anayeweza kutishia mtu au kuwaambia wanachama wengine wasimuunge mkono Aisha,” alisema.
Bw Omar aliwahakikishia wanachama wote wa UDA ulinzi wakitaka kutumia chama hicho kuwania nafasi za uongozi wa kisiasa.
Wakati huo huo, wanasiasa wa Pwani walimtetea Bi Jumwa dhidi ya viongozi wa Taasisi ya Wahandisi ya Kenya ambao wanapinga uteuzi wake.
Seneta wa Tana River, Bw Danson Mungatana, alisema Bi Jumwa ana uwezo na hakuna mtu atakayempinga.
“Hatuwezi kukubali kwamba kwa uteuzi wote wa wenyekiti katika nchi hii hakuna anayezungumza lakini inapohusu eneo la Pwani wanaanza kutuingilia na kutuvuruga,” alisema.
Bw Joho alisisitiza azma yake ya kuunganisha eneo la Pwani kisiasa.
Gavana huyo wa zamani wa Mombasa, alisema yuko tayari kwa kazi hiyo na kuwaonya wale wanaonuia kuvuruga mipango yake ya kuunganisha eneo hilo wakae kando.