2022: Mayatima wa 'Tangatanga'
Na WANDERI KAMAU
AGIZO la Rais Uhuru Kenyatta kwamba hakuna mwanasiasa yeyote atakayeruhusiwa kupiga siasa kabla ya mwaka wa 2022 limewaacha wanasiasa ambao wamekuwa wakiandamana na Naibu Rais William Ruto maarufu kama ‘Team Tanga Tanga’ katika njia-panda.
Wanasiasa hao wamekuwa wakiandamana na Dkt Ruto katika sehemu mbalimbali nchini “kuzindua” miradi ya maendeleo, huku wakimfanyia kampeni kama mwaniaji anayefaa zaidi kuchaguliwa kama rais na Wakenya mwaka huo.
Hata hivyo, hatua ya Dkt Ruto kujitenga na kundi hilo imewaacha wanasiasa hao katika mshangao, ikizingatiwa kuwa mbali na wengi wao kuapa kufanya kila wawezalo kuhakikisha kwamba amechaguliwa kama rais ifikapo 2022, baadhi wamekuwa wakiotea kuwa naibu wake.
Kundi hilo linajumuisha Kiongozi wa Wengi katika Seneti Kipchumba Murkomen, wabunge Kimani Ichung’wa (Kikuyu), Rigathi Gachagua (Mathira), Ndindi Nyoro (Kiharu), Moses Kuria (Gatundu Kusini), magavana Anne Waiguru (Kirinyaga), Mwangi wa Iria (Murang’a), Francis Kimemia (Nyandarua, kati ya wengine.
Kwenye taarifa yake, Ruto alikanusha kumpa ruhusa mwanasiasa yeyote kumfanyia kampeni ya urais, akisisitiza kuwa lengo lake ni kumuunga mkono Rais Kenyatta kutimiza Ajenda Nne Kuu za Maendeleo.
“Nimefahamu kwamba kuna kundi la watu wanaodai kunifanyia kampeni za urais mwaka 2022. Hata hivyo, hakuna wakati ambapo nishajihusisha wala kumruhusu yeyote kujihusisha katika kampeni hizo kwa niaba yangu. Mimi ni mwanademokrasia anayeamini kuwa kampeni zinafanywa wakati ufaao pekee,” akasema Dkt Ruto, kwenye taarifa iliyotolewa na msemaji wake, Bw David Mugonyi.
Mbali na hayo, Dkt Ruto aliwaambia wanasiasa hao “kutoa jina lake kwenye shughuli zozote zinazolingana na kampeni za mapema.”
Dkt Ruto pia alionekana kusisitiza hayo mnamo Jumamosi alipoandamana na Rais Kenyatta katika Kaunti ya Kajiado, aliposema kwamba sasa ataangazia masuala ya maendeleo.
“Siasa kando, ufisadi nyuma, maendeleo mbele. Sasa tutazingatia tu masuala ya maendeleo, kama alivyoagiza Rais (Uhuru). Tutafanya kampeni wakati wake ukifika,” akasema Dkt Ruto.
Wachanganuzi wanasema kuwa hatua hiyo ni pigo kubwa kwa wanasiasa hao, kwani baadhi yao wamekuwa wakitumia ziara na jina la Ruto kuimarisha mikakati yao ya kujinadi kama mgombea-mwenza wake, ikiwa atawania urais kwa tiketi ya Chama cha Jubilee (JP).
Aidha, baadhi yao wamekuwa wakionekana kupigania kuwa viongozi na wasemaji wa ukanda wa Mlima Kenya, ikiwa Rais Kenyatta atang’atuka kwenye uongozi wa kitaifa.
“Ni pigo kubwa kwao kisiasa, hasa baada ya Dkt Ruto mwenyewe kujitenga nao. Hili linamaanisha kwamba itabidi kutafuta majukwa mbadala kujijenga,” asema Prof Macharia Munene, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.
Wanasiasa hao wamekuwa wakimtetea vikali Dkt Ruto, wakimhakikishia kwamba eneo la Mlima Kenya litamuunga mkono kwa vyovyote vile.
Wengi walimtetea vikali hata wakati aliyekuwa Naibu Mwenyekiti wa JP David Murathe aliposema kwamba si lazima ukanda huo umuunge mkono Ruto uchaguzi huo ufikapo.