• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 6:55 AM
‘Siwezi kuwasamehe Dk Kwenye Beat na Hope Kid’

‘Siwezi kuwasamehe Dk Kwenye Beat na Hope Kid’

Na FRANCIS MUREITHI

MWANAMKE anayedai alidhulumiwa kimapenzi na wasanii wawili wa muziki wa injili jijini Nairobi amepuuza msamaha wa wasanii hao akisema ulitumwa kupitia mitandao ya kijamii na haukumrejelea moja kwa moja.?

Binti huyo wa miaka 20 kutoka Nakuru ambaye jina lake tumelibana kwa sababu za kisheria, amewalaumu wasanii hao, Dk Kwenye Beat na Hope Kid kwa kumlazimisha ashiriki ngono nao, kitendo kilichomwambukiza ugonjwa wa zinaa.

Msichana huyo pia amesema hatawasamehe wawili hao kwa kumshushia hadhi katika jamii, kumharibia maisha yake kisha kumtelekeza.

“Hili si suala la msamaha. Mimi bado nina makovu ya kile walinifanyia. Baada ya kuonja asali yangu wamenitelekeza na hata hawajali ninachopitia.”

“Mimi ninahitaji pesa za kutibu virusi walivyoniambukiza kwa jina Human Papillomvirus (HPV) vinavyosababisha kansa ya uzazi. Mimi hutumia Sh5,000 kununua dawa kila mwezi. Ninamtegemea ndugu yangu ambaye hawezi kunikimu kwa sababu pia ana familia yake,” akasema mwanamke huyo.

Vile vile alisema kwamba hatua ya wawili hao kuendelea kustarehe na kukimbilia mitandao ya kijamii kumwomba awasamehe ilhali hawajawasiliana naye ama kupendekeza njia za kumpa msaada kama kiburi kisichofaa kuvumiliwa.

“Dk Kwenye Beat na Hope Kid wanashiriki starehe zao bila kujali ninakotoa hela za kununua dawa ghali za kujitibu. Iwapo msamaha wao ni kweli basi wanafaa kunisaidia kugharamia dawa ninazohitaji.”

“Hakuna mahali katika msamaha wao wamenirejelea kwa jina kwa hivyo siwaamini kabisa. Kile nimesalia nacho ni kutubu mbele za Mwenyezi Mungu na kuiomba jamii msamaha,” akashikilia binti huyo.

DK Kwenye Beat ndiye alikuwa wa kwanza kujitosa katika mtandao ya kijamii kisha Hope Kid akafuata baadaye walipoandika msamaha wao.

“Ningependa kwanza kumwomba Mungu msamaha kwa kutenda dhambi. Pia ningependa kuomba msamaha kanisa langu, familia yangu, mashabiki wangu kwa kuwa mimi si binadamu mkamilifu.”

“Mimi ni mwanaume aliyetenda dhambi nyingi ila Mwenyezi Mungu amekuwa akiyabadilisha maisha yangu kila siku. Kwa masikitiko makuu, mambo haya yananifika wakati nilikuwa naendelea kubadilika,” akaandika DK Kwenye Beat.

Hope Kid naye aliandika hivi, “Nimekosa mbele ya Mwenyezi Mungu na binadamu. Nasikitika sana kwa wale ambao vitendo vyangu vimewaathiri kwa njia moja au nyingine. Nawaomba mnitilie dua ili niweze kubadilika kabisa na nisiyarudie makosa yangu,” akaandika.

Mwanamke huyo alifichua kwamba mchungaji wa Hope Kid ndiye alimpigia simu na kumrai arejee Nairobi ili akutane na Hope Kid mwenyewe ila akashikilia kwamba hawezi kufika jijini humo kwa mara nyingine kwa kuwa aliyotendewa na wanamuziki hao bado yanamhangaisha akilini.

Binti huyo pia alifichua kwamba bado haelewi kwa nini Hope Kid alimwambia aende jijini Nairobi kisha baadaye akabadili nia na kumpeleka katika nyumba DK Kwenye Beat ambako walimlazimisha kushiriki ngono nao.

“Mahangaiko na msongo wa kimawazo ninayopitia sasa ni kwasababu ya Hope Kid. Nimemtumia picha kuonyesha jinsi nilivyojikata kidoleni ili kumdhihirishia uchungu ninaopitia,” akafunguka huku akisema kwamba amemweleza mamake mzazi kuhusu kisa hicho japo babake bado yupo gizani kwa sababu hajui namna atakavyopata ujasiri na kumsimulia tukio lenyewe.

Wakati uo huo alimkemea DK Kwenye Beat kwa kumfokea mamake na kumtusi kwenye simu, video hiyo iliposambaa katika mtandao ya kijamii.

Hata hivyo amesema atawasamehe wasanii hao wawili na kutowashtaki mahakamani iwapo watakubali kugharimia matibabu yake na mambo mengine ya kimsingi.

Makubaliano hayo kulingana naye yataafikiwa mbele ya wakili kutoka Chama cha mawakili wanawake (FIDA) na itakuwa funzo kwa wasanii wengine wenye mazoea ya kuwanyanyasa mabinti kimapenzi bila  adhabu.

You can share this post!

2022: Mayatima wa ‘Tangatanga’

Moto wa karatasi wateketeza kiwanda cha gesi

adminleo