• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Magavana 40 waliajiri mawaziri bila kuzingatia sheria – EACC

Magavana 40 waliajiri mawaziri bila kuzingatia sheria – EACC

Na VITALIS KIMUTAI

MAGAVANA karibu 40 wamekosolewa na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kwa kukosa kutimiza mahitaji ya sheria za uongozi na maadili walipoajiri mawaziri katika kaunti zao.

Miongoni mwa magavana ambao mawaziri wao hawakuhojiwa na kuidhinishwa na EACC kabla ya kuajiriwa, ni Mwenyekiti wa Baraza la Magavana aliye pia Gavana wa Kakamega, Bw Wycliffe Oparanya, mtangulizi wake, Bw Josphat Nanok (Turkana), Naibu Mwenyekiti wa COG aliye pia Gavana wa Murang’a, Bw Mwangi Wa Iria na mtangulizi wake Bi Anne Waiguru (Kirinyaga).

Gavana wa Kwale, Bw Salim Mvurya na mwenzake wa Makueni, Prof Kivutha Kibwana pia wamo kwenye orodha hiyo.

Ufichuzi huu umetolewa wakati ambapo vita dhidi ya ufisadi vinavyoendelezwa na utawala wa Rais Uhuru Kenyatta, vinahitaji kiwango kikubwa cha maadili miongoni mwa watumishi wote wa umma.

Barua iliyoandikwa Januari 12, 2019, ikatiwa sahihi na Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria, Bw David Too kwa niaba ya Afisa Mkuu Mtendaji wa EACC inasema, “Tume imegundua uteuzi na uajiri wa mawaziri katika kaunti 40 haukufuata taratibu zinazohitajika. Uajiri wao haukutimiza mahitaji ya Kifungu cha Sita cha Katiba na Sheria ya Uongozi na Uadilifu ya 2012.”

Barua hiyo iliandikwa kwa Afisa Mkuu Mtendaji wa Baraza la Magavana, Bi Jackline Omogeni.

Ilionekana kulikuwa na barua nyingine iliyotumwa awali kwa baraza hilo kutoka kwa aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa EACC, Bw Halakhe Waqo mnamo Agosti 24, 2017 na kutumiwa makatibu wote na bodi za utumishi wa umma katika kaunti.

Sehemu ya 35(1) ya Sheria ya Serikali za Kaunti inahitaji kwamba mtu anayeajiriwa katika baraza la mawaziri la kaunti anafaa kutimiza mahitaji ya Kifungu cha Sita cha Katiba.

EACC inasema kila uteuzi unafaa kuandamwa na thibitisho la uadilifu, na hilo halikufanywa katika kaunti hizo 40.

Bw Waqo alikuwa ameagiza kwamba orodha ya wale wanaoteuliwa kuwa mawaziri katika kaunti iwasilishwe kwa EACC ili kufanyiwa utathmini, ingawa inavyoonekana agizo hilo lilipuuzwa na magavana, bodi za utumishi wa umma na mabunge ya kaunti.

Jukumu la kufuatilia suala hilo sasa liko mikononi mwa Bw Twalib Mubarak ambaye alichukua mahali pa Bw Waqo hivi majuzi.

You can share this post!

KANU yasifu agizo la Rais kukomesha siasa za 2022

Kaunti zisaidie kuendeleza lugha asili – Ngugi wa...

adminleo