Marwa: Tuko tayari kumaliza zogo la kanisa Adventista
NA CECIL ODONGO
VIONGOZI Waadventista wenye hadhi serikalini na katika jamii walitangaza kujitolea kwao kupatanisha kambi mbili zinazozozania uteuzi wa wanachama wa kamati ya kuwapendekeza wahudumu wa Kanisa la Kiadventista la Nairobi Central(Maxwell).
Tofauti kuhusu uanachama wa kamati hiyo zimekuwa zikiendelea tangu mwisho wa mwaka jana huku zikitishia kulemaza jinsi shughuli za kanisa hilo maarufu nchini zinavyoendeshwa na kulipaka tope machoni mwa maelfu ya waumini kote nchini.
Katibu katika wizara ya Ugatuzi Nelson Marwa akiwahutubia waumini kanisani humo Jumamosi, alieleza kutofurahishwa kwake na kuendelea kushamiri kwa utata huo na kuzitaka kambi mbili zinazozozana kukubaliana.
“Kanisa hili ni kama Kituo Kikuu cha Kanisa la Adventista nchini kwasababu kila mgeni anayeingia nchini huelekezwa kushiriki hapa. Ni aibu sana kwamba tunashindwa kutatua mambo kwa uaminifu na kuharibu jina la kanisa lenye hadhi kama hili. Kila mtu amekuwa akiniuliza kuhusu kinachoendelea Maxwell.”
“Nimezungumza na Waziri Fred Matiang’ na Jaji Mkuu David Maraga pamoja na watu wengine ili tuone jinsi tunavyoweza kuketi chini na kutatua tofauti hizi ndipo Maxwell irejelee hadhi yake ya zamani. Watu mashuhuri wakiwemo wabunge na viongozi wa juu katika taifa hili hushiriki hapa, ni aibu kubwa iwapo mambo kama haya yanatokea. Naomba tuabudu Mungu kwa ukweli na kwa uaminifu,” akasema Bw Marwa Jumamosi.
Utata kuhusu majina ya wanakamati umeanika wazi tofauti kali kati wachungaji wawili wa kanisa hilo na wazee ambao wamewalaumu kwa kutumia ukabila kama kigezo cha kuafika majina yaliyowasilishwa awali.
Hata hivyo, Pasta Jean Pierre Maiywa ambaye alihubiri siku ya Jumamosi alitangaza kwamba kamati iliyoteuliwa awali imefutiliwa mbali huku akikosa kubainisha ni lini kamati nyingine itateuliwa ili majina ya wahudumu wa mwaka huu yatangazwe.
“Kamati iliyopendekezwa imevunjiliwa mbali ili kupisha majadiliano. Hata hivyo nawaomba waumini wanye wito, msukomo na ari ya kulihudumia kanisa kuyawasilisha majina yao. Mniombe na tuliombee kanisa letu ili tuweze kuafikiana kuhusu suala hili,” akasema Pasta Maiywa.
Baadhi ya Waumini wa kanisa hilo wamekuwa wakionyesha kutoridhishwa na uongozi wa wachungaji hao na kuutaka usimamizi wa kanisa la adventista nchini kuwahamisha.
Kwa kipindi cha majuma mawili yaliyopita, wanaoung’unika wamekuwa wakiasi ibada na kushauriana kwa makundi nje ya kanisa hilo. Mkutano wa kujadili uongozi wa kanisa hilo pia ulisambaratika wiki mbili zilizopita baada ya muafaka kuhusu majina hayo kukosekana miongoni mwa waumini, wazee na wachungaji.