Chebukati alifariki na siri za sava za uchaguzi
IKIWA kuna siri kubwa ambayo Wafula Wanyonyi Chebukati, mwenyekiti (mstaafu) wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) aliyefariki jana alikosa kufichulia Wakenya, ni kwa nini alikataa kufungua sava alizotumia kwa kura ya urais katika uchaguzi mkuu wa 2022.
Suala hili lilizua mvutano kati ya tume na upinzani ambao ulishikilia kuwa, uchaguzi huo ulikumbwa na dosari na ni kufunguliwa kwa sava ambako kungethibitisha kilichotokea.
Bw Chebukati alikaa ngumu, akiungwa na muungano ulioshinda wa Kenya Kwanza ambao ulisema alisimamia uchaguzi uliokuwa huru na wa haki na kwamba, mchakato aliotumia ulikuwa sawa na kuweka sava wazi kwa Wakenya.
Wakili huyo aliyesimamia uchaguzi wa kwanza wa urais kubatilishwa na Mahakama mnamo wa 2017 na wa 2022 uliogawanya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ( IEBC) alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 63.Familia yake ilisema, alifariki Alhamisi saa tano usiku baada ya kuugua kwa muda.
Bw Chebukati alikamilisha kipindi chake cha miaka sita akiwa mwenyekiti wa IEBC mnamo Januari 17, 2023.Muhula wake kama Mwenyekiti wa IEBC ulianza Januari, 2017 kufuatia kuondolewa kwa Ahmed Issack Hassan na makamishna wenzake.
Wakili huyo alichukua wadhifa huo wakati uliojaa joto la kisiasa, huku kiongozi wa upinzani Raila Odinga akikabiliana na Rais Uhuru Kenyatta, ambaye alikuwa akigombea kwa muhula wa pili.
Ni siku chache kabla ya uchaguzi huo ambapo aliyekuwa meneja wa ICT wa IEBC, Chris Musando aliuawa na kufikia sasa hakuna aliyewajibishwa kwa mauaji yake. Bw Chebukati alilaani vikali mauaji ya Musando.
Bw Chebukati na kikosi chake walitwikwa jukumu la kuendesha mojawapo ya uchaguzi uliokuwa na ushindani mkubwa nchini Kenya ambao waliandaa kwa muda wa chini ya miezi saba.
Hata hivyo, uchaguzi wake wa kwanza kusimamia ulipingwa na matokeo ya kura za urais mnamo 2017 yakabatilishwa na Mahakama ya Juu katika uamuzi wa kihistoria.
Katika uamuzi wake, Mahakama ya Juu, wakati huo ikiongozwa na Jaji Mkuu David Maraga, iligundua kuwa uchaguzi alioshinda Uhuru Kenyatta dhidi ya Raila Odinga ulikumbwa na dosari na ukiukaji wa sheria huku ikilaumu IEBC.
Mahakama ya Juu iliamuru uchaguzi wa marudio wa urais ufanyike ndani ya siku 60. Hata hivyo, kiongozi wa upinzani Raila Odinga alisusia uchaguzi wa marudio, akisema hangeweza kushiriki uchaguzi uliosimamiwa na timu ile ile ‘iliyovuruga’ ule wa awali.
Pengine siri ya pili ambayo Chebukati alikufa bila kuelezea Wakenya ni sababu hasa ya kutofautiana na manaibu wake na baadhi ya makamishna mara mbili katika muhula wake katika IEBC, na hasa punde na baada ya uchaguzi.Mara kwa mara, Bw Chebukati alizozana na mirengo ya kisiasa lakini alipinga wito wa kujiuzulu.
Uchaguzi wa urais wa 2022 haukuwa tofauti, kwani upinzani ulidai mgombeaji wao, Bw Odinga, alitapeliwa na William Ruto kupendelewa.Upinzani, ambao ulipinga matokeo ya kura katika Mahakama ya Juu bila kufaulu, ulidai kuwa mfumo wa tume hiyo uliruhusu baadhi ya watu kuhujumu matokeo ya mwisho ili kumpendelea Dkt Ruto.
Hata hivyo, Mahakama ya Juu ilitupilia mbali madai hayo na kuidhinisha ushindi wa Dkt Ruto, ikitaja baadhi ya madai katika kesi kuwa ‘hewa’.Katika maandalizi ya uchaguzi wa Agosti 2022, na wakati wa kujumlisha kura, mzozo mkali wa ndani ulikumba tume, na kusababisha mgawanyiko kati ya makamishna.
Makamishna saba waligawanyika katika makundi mawili: moja likiongozwa na Bw Chebukati, Boya Molu, na Abdi Guliye, na lingine likiwa na naibu mwenyekiti Juliana Cherera, Francis Wanderi, Irene Masit na Justus Nyang’aya.
Vita baridi ndani ya IEBC viliendelea, lakini vililipuka hatimaye makamishna wanne walipopinga hadharani kuwasilishwa kwa matokeo ya uchaguzi wa urais.Makamishna Francis Wanderi, Irene Masit, Justus Nyang’aya na Makamu Mwenyekiti Juliana Cherera walipinga baadhi ya matokeo yaliyotangazwa na Bw Chebukati wakidai hayakuwa yamethibitishwa na makamishna wote.
Makamishna waliojitenga waliondoka Bomas of Kenya na kufanya mkutano na waandishi wa habari katika Hoteli ya Serena, ambapo walijitenga na matokeo ya urais yaliyotangazwa na tume.Walimkashifu Bw Chebukati kwa kupuuza mapendekezo yao wakisema kuwa alijiteua kuwa afisa wa kitaifa wa uchaguzi wa urais.
Mwenyekiti huyo alishinda kwa kuwa baada ya mvutano, makamishna waliompinga, ambao walifahamika kama Cherera Four, waliondoka kwenye tume hiyo huku mmoja wao, Bi Masit, akitimuliwa baada ya jopo la mahakama kubuniwa kuchunguza utendakazi wake.
Bw Chebukati alikuwa amelaumiwa na makamisha hao kwa kujaribu kuwaingiza raia wawili wa Venezuela, ambao walikamatwa katika uwanja wa ndege wakiwa na vifaa vya uchaguzi. Kulingana na Irene Masit, mmoja wa Makamishna hao, Bw Chebukati pekee ndiye alijua kuhusu raia hao na Makamishna hao walikuwa gizani.
Alisema: ‘Sikuwa na habari kuhusu ujio wa raia hao wa kigeni wakiwa na nyenzo za uchaguzi na hilo halikufikishwa kwa makamishna.”Baadaye, Agosti 17, 2022, Chebukati alidai katika taarifa kwa vyombo vya habari kwamba, makamishna wanne walikuwa wamejaribu kulazimisha marudio ya uchaguzi wa urais.Ingawa baadhi walimwona Bw Chebukati kama kiongozi aliyekuwa na kichwa ngumu, wengine walimwona kama mtu thabiti, asiyeyumbishwa na shinikizo kutoka nje.
Baada ya kuondoka madarakani mwishoni mwa muhula wake wa miaka sita, Bw Chebukati hakuonekana hadharani, huku ripoti zikisema kuwa afya yake ilikuwa ikidorora.Bw Chebukati aliyezaliwa Desemba 19, 1961, alikuwa na Shahada ya Kwanza ya Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi, na Uzamili katika Usimamizi wa Biashara kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta.
Alikuwa mwanasiasa na mwanachama wa chama cha Orange Democratic Movement lakini alijiuzulu kabla ya kutuma maombi ya kuwa Mwenyekiti wa IEBC. Mnamo 2007, aligombea kiti cha eneobunge la Saboti na kuibuka wa pili.