Jamvi La Siasa

Kalonzo ana imani Baba atakataa minofu ya Ruto na kurejea Upinzani

Na BENSON MATHEKA February 23rd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KIONGOZI wa Chama cha Wiper Kalonzo Musyoka anaonekana kuendelea kuota akitarajia mwenzake wa ODM Raila Odinga atakataa minofu anayorushiwa na Rais William Ruto na kurejea katika upinzani.

Licha ya ODM kushirikishwa katika Serikali Jumuishi, Bw Musyoka anatilia shaka uwezekano wa Raila kukubali wadhifa wa waziri mkuu ambao washirika wa karibu wa rais wanapendekeza apewe kupitia utekelezaji wa ripoti ya Kamati ya Mdahalo wa Kitaifa (NADCO).

Washirika wa Rais Ruto wakiongozwa na Seneta wa Nandi Samson Cherargei na mbunge wa Belgut Nelson Koech wanasisitiza kuwa baada ya Raila kushindwa katika uchaguzi wa mwenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika (AUC) anafaa kuteuliwa waziri mkuu nchini.

Katika taarifa aliyochapishwa kwenye akaunti yake ya X mnamo Februari 17, 2025 na baadaye akairudia ndani ya seneti, Cherargei alitaka utekelezaji kamili wa Ripoti ya NADCO kupitia marekebisho ya katiba.

“Lazima sasa tutekeleze kikamilifu Ripoti ya NADCO kwa kurekebisha Katiba ya 2010 ili kuunda ofisi ya Waziri Mkuu na kuruhusu Mheshimiwa Baba Raila Odinga kuhudumia Wakenya katika wadhifa huo,” Cherargei alisema huku akisisitiza umuhimu wa kutumia tajriba ya Raila.

“Hatuwezi kuruhusu uongozi bora na uzoefu wa Raila upotee jinsi Umoja wa Afrika ulivyofanya. Hii ndiyo njia ya pekee tunaweza kumthamini na kumtuza kwa kupigania utawala wa sheria na demokrasia nchini Kenya,” aliongeza.

Bw Koech aliunga mkono maoni ya Cherargei, akitoa wito kwa muungano unaotawala wa Kenya Kwanza kuunda nafasi inayofaa kwa Odinga serikalini.

“Raila Odinga anarejea nyumbani. Raila Odinga atakuwa akifanya nini kwa nguvu zake, kwa busara zake, kwa tajriba yake? Nadhani sisi katika Kenya Kwanza tunapaswa kumpa kazi. Uzoefu huo na ushauri ambao atatupa utasaidia katika kuboresha nchi yetu, jamii yetu na usimamizi wetu,” Koech alisema na kupendekeza ripoti ya NADCO kama mfumo wa kuunda wadhifa ambao utamfaa Odinga.

Hata hivyo, Bw Musyoka alionekana kuwa na maoni tofauti akishangaa Raila ataambia nini nchi, iwapo atakubali wadhifa huo bila kukitwa katika katiba ipasavyo.

Kulingana na Kalonzo, wanaosisitiza Raila apewe wadhifa huo, hawamjui Raila alisema ni kinyume cha katiba na kwamba kuukubali kutaathiri msimamo wa kisiasa wa Odinga.

“Wanasema Raila Odinga awe Waziri Mkuu? Hawamjui. Kulingana na yeye, na kulingana na sisi, yeye na Martha Karua walishinda uchaguzi, na sasa anataka awe Waziri Mkuu? Atakuwa anaiambia nini nchi?”Kalonzo alihoji.

Kulingana na Kalonzo, kukubali wadhifa huo pia kutamfanya Raila apoteze fursa ya kuhudumu kama kinara wa kushauriana na Rais William Ruto jinsi walivyokubaliana katika ripoti ya Kamati ya Kitaifa ya Mazungumzo (Nadco).

“Kitu pekee ninachotarajia ni kwamba Raila hatajiunga na Ruto. Akifanya hivyo, atapoteza nafasi ya kinara tuliyojita katika Nadco awe akishauriana na Ruto, hii ni sababu mojawapo Raila hawezi kujiunga na Ruto,” akaongeza.

Hata hivyo, wachanganuzi wa siasa wanasema Kalonzo amebaki katika ndoto kwamba Raila atamuunga mkono ilhali dalili ziko wazi kuwa kiongozi huyo wa ODM amekita ukuruba wake na Rais Ruto.

“Kalonzo hagutuki. Raila na Ruto wameshajipanga. Nafasi ya kutimia kwa ndoto zake kwamba hali itabadilika ni finyu sana,” asema mchambuzi wa siasa Katua Kioko.

Anasema hakuna kinachozuia Raila kukubali wadhifa mkubwa serikalini.

“Nafasi ya Raila kuwa rais katika uchaguzi mkuu wa 2027 imefifia na kwa sasa nyota yake ya kisiasa inaweza kuangaza tu akiwa karibu na Rais Ruto,” akasema.

Hata hivyo, alisema Raila anaweza kubadilisha mawimbi ya siasa wakati wowote kuelekea maslahi yake.