Mabadiliko ya Gachagua yashangaza
BW Rigathi Gachagua amebadilika kutoka Naibu Rais miaka miwili iliyopita hadi mwanasiasa aliyetimuliwa mamlakani na sasa kigogo wa siasa za eneo la Mlima Kenya anayepania kuhakikisha kuwa bosi wake wa zamani Rais William Ruto anatimuliwa mamlakani 2027.
Bw Gachagua amegeuka kuwa mkosoaji mkubwa wa serikali aliyosaidia kuundwa kwake huku akienda kinyume na kauli alizotoa awali kuhusu sera na mipango yake.
Wiki hii akikutana kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka na kiongozi wa DAP-Kenya Eugene Wamalwa kwa lengo la kusuka muungano mpya wa kisiasa, Gachagua alionekana kama mwanasiasa tofauti na yule aliyewashambulia vikali wawili hao kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022, akiwa mgombeaji mwenza wa Dkt Ruto.
Aliendelea kuwashambulia Mabw Musyoka na Wamalwa pindi alipoapishwa kuwa Naibu Rais baada ya Kenya Kwanza kushinda uchaguzi wa urais.
Kwa mfano mnamo Agosti 2023, Bw Gachagua aliwaambia waombolezaji wakati wa mazishi ya Mama Anne Kalekye, mamaka Mbunge wa Mwala Vincent Kawaya, eneo la Mwala, kaunti ya Machakos, kwamba wakazi wa eneo hilo wanapaswa kumtelekeza Bw Musyoka kwa kuwapotosha.
Yeye na Bw Musyoka sasa ni wandani wa kisiasa.Hata hivyo, mtu ambaye ameathirika zaidi na mabadiliko ya Bw Gachagua kisiasa ni Rais Ruto ambaye amekuwa akimshambulia vikali ndani ya miezi mitano iliyopita.
Huyu ndiye Gachagua ambaye aliwahi kumsifia Dkt Ruto kama “mtu mwaminifu ambaye sikuhitaji kuwekeana naye makubaliano kwa maandishi kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.”
Leo, mawazoni mwa Bw Gachagua Rais Ruto aliyemsifia kuwa kiongozi “anayejali masuala yanayowahusu wananchi wa kawaida na anayepingwa na watu wenye wivu pekee, sasa ni msaliti anayestahili kukataliwa debeni 2027.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta Charles Mwangi anataja hali hiyo kama uhalisia wa mambo katika siasa.“Hivi ndivyo hali ilivyo katika siasa ambapo mashindano ni kama mahusiano ya kimapenzi, ambapo watu hukosana na kutusiana unapotamatika,” anaeleza.
“Ni sawa kwa Gachagua kubadilisha misimamo yake baada ya muda, haswa yale mazuri aliyosema kuhusu Rais Ruto na serikali yalichangia kutimuliwa kwake Oktoba, 2024,” Dkt Mwangi anaongeza akisema kuwa hali hii huenda ikamsaidia Bw Gachagua kujifufua tena kisiasa.
Kwa mfano, awali Bw Gachagua aliunga mkono mpango wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu, akidai utazalisha nafasi za ajira kwa mamilioni ya vijana, lakini sasa amegeuka kuwa mpinzani mkubwa wa mpango huo.

“Wale wanaomkashifu Rais kuhusu mpango wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu hawaelewi manufaa ya ajenda hiyo kwa taifa hili,” akasema mnamo Machi 9, 2023 katika kaunti ya Murang’a.
Aidha, huku akionekana kumlenga Raila Odinga, Bw Gachagua aliwahi kusema serikali inalenga kuhakikisha kuwa wananchi wanaoishi katika nyumba nzuri na “hatuwezi kuwasikiza wanasiasa ambao furaha yao ni kuhakikisha kuwa watu wanaishi katika mitaa ya mabanda ili wawapigie kura miaka nenda miaka rudi.”
Lakini nyakati hizi Bw Gachagua anaamini kuwa mpango huo wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu unapasa kusitishwa akiutaja kama “sakata kubwa zaidi kuwahi kutokea katika utawala wa Rais Ruto.”
Kulingana na Mbunge huyo wa zamani wa Mathira, mpango huo ni njama ya kupata soko kwa bidhaa kama simiti, vyuma na mabati zinazotengenezwa na watu wenye uhusiano wa karibu na wakuu katika serikali hii.
Vile vile, baada ya Bw Odinga kupoteza katika uchaguzi wa uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) juzi, Bw Gachagua alitumia maneno matamu kumsifia akisema “Japo Afrika ilikuhitaji, Wakenya wangali wanakuhitaji zaidi, kama mwana wao mpendwa, ili uwasaidie kupambana na utawala huu dhalimu.”
Bima mpya ya Afya ya Kijamii (SHIF) ambayo Bw Gachagua aliwahi kuunga mkono, akiwa Naibu Rais, sasa ameitaja kama mpango uliofeli ulioanzishwa kwa lengo la “kufyonza Sh100 bilioni za kuweka mfumo mpya wa kuitekeleza badala ya kurekebisha mfumo wa NHIF.”