Msife moyo, ligi haijaenda, Slot atuliza Wanabunduki
LICHA ya mashabiki wa Arsenal kufa moyo na kusema Liverpool sasa ipewe ubingwa wa Ligi Kuu, kocha Arne Slot anasema vijana wake bado wana safari ndefu.
Liverpool walikung’uta Newcastle 2-0 kupitia mabao ya Dominik Szoboszlai na Alexis Mac Allister ugani Anfield mnamo Jumatano.
Reds wamefungua pengo la alama 13 juu ya jedwali dhidi ya wapinzani wa karibu Arsenal walioumiza nyasi bure katika sare tasa mikononi mwa wenyeji Nottingham Forest.
“Bado safari ni ndefu kabla ya kuanza kusherehekea. Tunasalia na michuano 10 ya ligi pamoja na majukumu ya fainali ya League Cup na mipepetano miwili muhimu dhidi ya Paris Saint-Germain,” akasema Slot.
Liverpool sasa wamefunga mabao mawili ama zaidi katika mechi 18 mfululizo ugani Anfield katika mashindano yote; ambayo ni rekodi ndefu ya zaidi ya bao moja nyumbani kwa klabu ya EPL, tangu Sunderland kutoka Februari hadi Desemba 1935.
Mabingwa hao wa zamani pia sasa hawajapoteza mechi 24 za ligi — rekodi ambayo ni ya tatu kwa ubora kwa Liverpool, baada ya michuano 31 kati ya Mei 1987 na Machi 1988 na mikwaruzano 44 kutoka Januari 2019 hadi Februari 2020.
Reds watakabana koo na PSG kwenye Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) katika raundi ya 16-bora mnamo Machi 5 (Parc des Princes) na Machi 11 (Anfield), Southampton ligini (Anfield) na Newcastle katika fainali ya League Cup mnamo Machi 16 (Wembley).
Arsenal nao walishuhudia masaibu yao yakiongezeka ambapo sasa hawajafunga bao katika mechi mbili mfululizo za ligi tangu Mei 2023.
Kwa kupiga sare ya 0-0, Forest nayo ilimaliza rekodi ya mechi 56 ya sare za kufungana angalau bao moja.
“Inasikitisha hatukupiga Forest. Hata hivyo, naona kidogo tuliimarika kuliko tulivyokuwa dhidi ya West Ham,” akasema kocha wa Arsenal, Mikel Arteta.
Katika mechi nyingine, wenyeji Brentford walitupa uongozi wakitoka 1-1 na Everton.
Yoane Wissa alitetemesha nyavu za Toffees kabla ya mapumziko, huku Jake O’Brien akisawazisha dakika ya 77.