Dimba

Benni McCarthy aliyehangaika Man United kutambulishwa kama kocha mpya Harambee Stars

Na CECIL ODONGO February 28th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

JAGINA wa Afrika Kusini Benni McCarthy aliwasili nchini Kenya mnamo Alhamisi huku hafla ya kutambulishwa kwake rasmi kama kocha wa timu ya taifa Harambee Stars, ikiratibiwa kufanyika Jumatatu.

McCarthy atachukua mikoba kutoka kwa Francis Kimanzi ambaye amekuwa kaimu kocha tangu Desemba 11. Alikuwa akishikilia nafasi hiyo baada ya kutimuliwa kwa kocha raia wa Uturuki Engin Firat.

Kimanzi aliongoza Kenya kunogesha kipute cha Mapinduzi Cup katika Kisiwa cha Zanzibar mapema Januari. Atakuwa katika kikundi kitakachosaidia McCarthy kufahamiana vyema na wachezaji ili kufanya kazi yake ipasavyo.

Kocha Francis Kimanzi aliposimamia Harambee, katika kikao na wanahabari kuhusu Mapinduzi Cup Kisiwani Zanzibar mnamo Januari 6, 2025. PICHA | FKF

Firat alijiuzulu akilalamikia kutolipwa kwa mshahara wake wa miezi 13 na uliokuwa uongozi wa Shirikisho la Soka Nchini (FKF) chini ya Nick Mwendwa.

Rais wa FKF Hussein Mohamed wiki hii alithibitisha uteuzi wa McCarthy kama kocha wa Stars na akaonyesha imani kuhusu uwezo wake wa kuchapa kazi.

“Amehitimu vizuri na nina imani atatambisha timu yetu kungáa kwenye mashindano mbalimbali,” akasema Mohamed.

Duru kutoka FKF ziliarifu kuwa McCarthy atatambulishwa rasmi pamoja na naibu wake na kocha mwingine msaidizi katika sherehe itakayofanyika jumba la mikutano la KICC jijini Nairobi.

“Baada ya kocha na benchi yake kuzoea kazi, Kimanzi atapokezwa wadhifa mwingine ambao aliahidiwa alipokubali kushikilia usukani wa ukocha,” zilisema duru hizo.

McCarthy, 47, amepewa kandarasi ambayo itadumu hadi Oktoba 13 wakati mechi za kufuzu Kombe la Dunia 2026 zitakamilika.

Hapo ndipo FKF itaamua iwapo ataendelea kuifunza Harambee Stars au kama watasaka kocha mwingine.

McCarthy wakati akinoa klabu ya AmaZulu FC inayoshiriki Ligi Kuu ya Afrika Kusini. PICHA | MAKTABA

Kibarua cha kwanza cha McCarthy itakuwa pale Kenya ikivaana na Gambia Machi 17 kisha Gabon Machi 24. Kikosi kinatarajiwa kuingia kambini wiki ya kwanza ya Machi.

McCarthy ana rekodi ya kumezewa mate kwani amechezea klabu kadhaa kubwa kama vile Ajax ya Ligi Kuu Uholanzi (Eredivisie), Celta Vigo ya Uhispania (La Liga), Porto ya Ureno (Primeira Liga), Blackburn Rovers na West Ham za Uingereza (EPL) pamoja na Orlando Pirates ya Afrika Kusini (PSL).

Amechezea Afrika Kusini mechi 79 na kufungia Bafana Bafana mabao 31, akishikilia rekodi ya kufunga mabao nchini humo.

Timu ya mwisho aliyoifunza ni Manchester United ambapo alikuwa msaidizi wa Erik ten Hag kati ya 2020-2024.

Pia amewahi kuzinoa Cape Town City na AmaZulu kama kocha mkuu na Sint-Truiden naibu kocha, zote zinazoshiriki Ligi Kuu ya Afrika Kusini (PSL).

Katika mechi za kufuzu Kombe la Dunia 2026, Kenya inayoyomea katika nafasi ya nne na alama tano kwenye Kundi F baada ya kusakata mechi nne.

Cote d’Ivoire maarufu Ivory Coast inaongoza kundi na alama 10 ikifuatiwa na Gabon (9), Burundi (4), Gambia (3) kisha Ushelisheli sufuri.