MAWAIDHA YA KIISLAMU: Karibu mgeni wetu Ramadhan hii ya mwaka 2025
KWA jina la Mwenyezi Mungu mwenye kuneemesha neema kubwa kubwa na neema ndogo ndogo. Tumejaaliwa siku hii tukufu, bora na aula ili kuambizana na kukumbushana kulihusu neno lake Mwenyezi Mungu.
Ama baada ya kumtukuza na kumshukuru mwisho wa shukrani Muumba wetu, Allah (SWT), pia tunachukua satua na uzito wa nafasi hii kumtilia dua mwombezi wetu, Mtume (SAW), pamoja na Maswahaba, aila yake yote na ahali zake.
Leo hii ndugu yangu tunazungumza nawe muumin wa dini hii tukufu ya Kiislamu tukiwa katika hoi hoi, sherehe, nderemo za kuulaki mwezi mwingine mtukufu wa Ramadhan.
Mwezi mtukufu mno. Utukufu huu ukitokana na twawabu tele na kila aina ya malipo yaliopo kwenye ibada za mwezi huu. Mwezi ambao tunajua wazi kuwa hata ibada ya sunna inalipwa kama faradhi. Mwezi umegawika katika makumi matatu ya kuchuma thawabu. Mwezi ambao upo usiku mtukufu almaarufu Lailatul-Qadr.
Ni yetu matumaini kuwa sisi ambao tutajaaliwa kuufunga mwezi huu wa Ramadhan, dua na maombi yetu pamoja na saumu zetu zitatakabaliwa. Na wale ambao ndugu zetu tuliofunga nao mwezi jana, mwezi wa Ramadhan, na hawakujaaliwa kuuona mwezi huu, tunawatilia dua. Na wale ambao pia hatutojaaliwa kuumaliza mwezi huu wa Ramadhan tuwe na hatima njema.
Ibada hii ya utukufu wa Ramadhan ituweke karibu sana na Mola wetu na kusalia katika ibada hata baada ya kuondoka mwezi huu wa fadhila na kuweka mbali na moto wa Jahanaam. Aidha, dunia nzima, In Shaa Allah, itautumia mwezi huu kuhubiri amani, Subira na kustahamiliana katika ardhi hii ya Mwenyezi Mungu.
Alhamdulillahi kila dalili zinaoenesha kuwa angalau ndugu zetu huko Gaza watapata afueni ya saumu mwaka huu ikilinganishwa na saumu ya mwaka jana. Vivyo hivyo, amani na nusra zipatikane katika maeneo yote duniani. Kwa wale ambao hawataweza kufunga kutokana na sababu ambazo zimeruhusiwa kidini, twaomba Allah (SWT) awajaalie waweze kutekeleza ibada nyinginezo ambazo zinaambatana na funga ya saumu.
Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu kwenye Kurani sura ya Al-Baqarah aya ya 183: “Enyi Mlioamini! Mmelazimishwa kufunga (Saumu) kama walivyolazimishwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha Mungu.”
Ni yetu matumaini kuwa asasi na taasisi husika zitatupa sisi waumini wa dini hii tukufu ya Kiislamu wakati mwepesi na mazingira mwafaka ya kutekeleza ibada hii, hasa usalama wa kutosha kwenye ibada na swala za usiku.
Ijumaa Mubarak.