Makala

Kenya yageuka uwanja wa wageni haramu

Na  VITALIS KIMUTAI March 1st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

RAIA wa kigeni wamevamia miji mikubwa ya Kenya wakiendesha biashara ndogo ndogo katikati na viungani mwa miji hiyo.

Watu hao hasa wa asili ya Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) huuza bidhaa kama vile nguo, vipuri vya simu, viatu, mboga na matunda huku wengine wakihudumu kwenye vibanda vya kunyoa na saluni.

Katika miji midogo, baada ya wenyeji kufunga biashara zao, wageni hawa huhiari kuendelea na biashara hadi usiku wa manane kuhakikisha wanawafikia wateja wote.

Katika jiji kuu la Nairobi, wageni hao wanaendesha biashara katika maeneo ya Gikomba, Eastleigh, Kasarani na Muthurwa, wakiuza kila kitu zikiwemo nguo za mitumba na bidhaa za nyumbani.

Mjini Kisumu, raia hao wa kigeni wanaendesha biashara katikati ya mji na mitaa mbalimbali huku katika miji ya Bomet na Nakuru uwezo wao wa kufanya kazi kwa saa nyingi ukiwawezesha kunawiri zaidi katika biashara ya uchuuzi.

Katika mji wa Kitengela, raia wa DRC wamebuni ushirikiano wa karibu zaidi kiasi kwamba wenyeji hurejelea mitaa wanakoishi kama “Kinshasa Ndogo”.

Lakini sasa baadhi ya wachuuzi wa asili ya Kenya wameanza kulalamika kuwa biashara zao zinaharibiwa na wageni hawa ambao huhiari kupata faida ndogo.

Maafisa wa serikali za kaunti pia wamejipata na kibarua cha kudhibiti idadi kubwa ya wafanyabiashara hao wa kigeni ambao biashara zao hazijasajiliwa rasmi.

Hali hiyo inachangia serikali hizo kufeli kukusanya ushuru na ada nyinginezo kutoka kwa wageni hao.Licha ya maafisa wa serikali hizi kuendesha misako dhidi ya wachuuzi hawa haramu, huwa wanabuni mbinu nyingine za kukwepa mitego ya maafisa hao.

Uchumi thabiti wa Kenya, ulinzi dhaifu mipakani na sera legevu za kuingia nchini zimechangia nchi hii kuwa kivutio kwa wahamiaji haramu wanaosaka nafasi za kujistawisha kiuchumi.

Jiji la Nairobi limegeuka kuwa kitovu cha wahamiaji wanaotoroka maisha magumu katika nchi zao.Wageni wengi wasiosajiliwa, hasa kutoka mataifa ya Mashariki na Kati ya Afrika wametwaa nafasi za ajira ambazo kimsingi zinapaswa kujazwa na wenyeji.

Takwimu kutoka kwa Idara ya Uhamiaji zinaonyesha kuwa kati ya miaka ya 2023 na 2024, jumla ya wahamiaji 1,455 wasiosajiliwa walikamatwa nchini. Mnamo 2022, jumla ya wahamiaji 1, 219 walinaswa baada ya kupatikana bila kibali cha kuwaruhusu kuwa nchini.

Wengi wao wamerejeshwa katika nchi zao lakini wengine wakarejea nchini tena, hali inayoibua wasiwasi kuhusu kiwango cha ulinzi mipakani. Kwa mfano, mnamo Februari 16, jumla ya raia 18 wa Burundi walinaswa katika kaunti ya Bomet wakiwa njiani kuelekea Nairobi.

Maafisa wa usalama wanaamini kuwa watu hao walikuwa njiani kuungana na maajenti kabla ya kujiunga na jamii ya wahamiaji haramu nchini Kenya.Polisi wanasema kuwa gari aina ya minibus ambalo wageni hao walikuwa wakisafiria lilisimamishwa katika kizuizi cha barabara ya Bomet-Kaplong.

Watu hao, watu wazima 16 na watoto wawili, walifikishwa katika mahakama moja ya Bomet ambapo walikiri kosa la kuwa Kenya kinyume cha sheria.Baada ya raia hao wa Burundi kuzuiliwa kwa wiki moja, Hakimu Mkuu Esther Boke aliagiza kuwa warejeshwe nchini mwao.

Licha ya uwepo wa hatari ya wao kukamatwa kwa kuwa nchini kinyume cha sheria, wageni ambao tulizungumza nao walisema kuwa wataendelea kuendesha biashara zao nchini.
 Peter*, mchuuzi kutoka DRC anayeendesha shughuli zake mjini Bomet anasema ameishi Kenya kwa miaka mitatu na hana mipango ya kurejea nyumbani kwao.

“Kwa mtazamo wetu raia wa Congo, Kenya ni kama ahera…. Kenya ni kama Amerika. Ni nchi yenye nafasi nyingi ya mtu kujistawishaji. Watu wa huku wazuri na ni nadra kwetu kuitishwa stakabadhi zozote za utambulisho,” akasema.

Lakini sawa na wachuuzi wenzake ambao sio Wakenya, Peter alidinda kufichua jinsia aliweza kupata nambari ya simu ya mkononi.

Lakini uchunguzi zaidi wa Taifa Leo ulibaini kuwa laini yake ya simu ya mkononi imesajiliwa kwa jina la mwanamke mmoja Mkenya; kutokana na maelezo kwenye M-Pesa baada ya kulipia bidhaa anazouza.