Jamvi La Siasa

Raila ageuza mbinu aacha mapambano ya maandamano

Na  BENSON MATHEKA March 2nd, 2025 Kusoma ni dakika: 3

KIONGOZI wa ODM Raila Odinga ameacha maandamano barabarani na siasa za mapambano makali na badala yake amekumbatia mazungumzo kutatua matatizo yanayokabili Wakenya.

Kwa miaka mingi, Raila alifahamika kwa kuambia wafuasi wake wasilale waendelee kupambana hasa alipohisi kwamba hakushindwa kwa haki katika uchaguzi wa urais ambao amegombea mara tano bila kufaulu.

Vile vile, amekuwa akiitisha maandamano kulalamikia sera za serikali zinazokandamiza na kunyanyasa raia.Wadadisi wa siasa wanasema kwamba baada ya kushindwa kutwaa urais mara tano na umri wake ukiwa zaidi ya miaka 80, Bw Odinga amebadilisha mbinu na ndio sababu anashirikiana na Rais William Ruto kwa lengo ya kufurahia minofu ya serikali huku akisisitiza hatua anazochukua ni kwa manufaa ya raia.

Baada ya kushindwa katika uchaguzi wa mwenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika (AUC),Bw Odinga amenukuliwa akisema kwamba atatangaza mwelekeo wa kisiasa wiki ijayo huku duru zikisema tayari amekamilisha mipango ya kuungana rasmi na chama tawala cha UDA cha Rais William Ruto.

Mnamo Ijumaa akiwa Busia, Bw Odinga alisema chama chake kitaendelea kupigania haki za Wakenya kupitia mashauriano.’Nitaendelea kushauriana ili kuhakikisha kwamba tunachukua mwelekeo utakaotanguliza mahitaji na haki za Wakenya.

Hatutakuwa na mzaha. Chama chetu kina mwelekeo. Hatuwafuati watu kwa upofu na bila mpango, tunafanya hivyo kwa sababu. ODM ina maadili yake na tutaendelea kupigania haki na maslahi ya raia,” alisema.

Hata hivyo, wadadisi wa siasa wanasema anachofanya Raila katika mikutano anayoita ya mashauriano ni kutetea uamuzi wake wa kushirikiana na Ruto.

“Usimtarajie Raila kurudi barabarani kuandamana au kuitisha maandamano. Anafahamu kuwa nguvu zinamuishia umri unavyosonga na anachofanya sasa ni kutumia fursa iliyojitokeza kuwa serikalini kupitia wanachoita Serikali Jumuishi,” anasema mdadasi wa siasa Musili Kioko.

Akiwa Kisumu Jumatano wiki hii alipokutana na viongozi wa ODM kutoka Nyanza, Bw Odinga alisema atakumbatia mazungumzo huku baadhi ya wanachama wenye misimamo mikali kama Gavana wa Siaya James Orengo akisema watakumbatia mazungumzo yaliyopangwa na pande zote ikiwemo serikali.

Bw Orengo na Katibu Mkuu wa chama hicho Edwin Sifuna walisema watafuata mwelekeo ambao Raila atawapatia japo wamekuwa wakipinga ODM kushirikiana na serikali ya Ruto.

Hata hivyo, wachanganuzi wa siasa na washirika wa karibu wa Raila wanasema ameamua kufanya kazi na Rais Ruto.Kulingana na wandani wa waziri mkuu huyo wa zamani, Raila ameamua kwamba atakuwa akitumia mazungumzo badala ya kuitisha maandamano yanayosambabisha wafuasi wake kuuawa.

“Kiongozi wa chama chetu cha ODM ameamua, na tunakubaliana naye, kutumia njia mpya za kutatua masuala yanayozua utata, akisisitiza haja ya mazungumzo badala ya maandamano ya mara kwa mara,” alisema afisa mmoja wa chama hicho cha chungwa, ambaye aliomba tusitaje jina kwa kuwa haruhusiwi kuzungumza kwa niaba ya Raila na chama.

Mbunge wa Kisumu Magharibi Rosa Buyu aliunga kauli hii katika mahojiano na kituo kimoja cha runinga Alhamisi akisema kuwa chama hicho kitakumbatia mwelekeo na mbinu mpya badala ya maandamano.

“Tumekuwa barabarani kuandamana kupigania mabadiliko; tunajua nini kinatokea. Alichosema Raila Odinga ni kwamba watu sasa wanazungumza. Watu sasa wanazungumzia SHA, ufisadi na mambo mengine. Swali ni sasa iwapo kuna njia bora ya kuua paka. Huko nyuma, tumeona vifo na familia zikilia kutokana na maandamano haya. Tunajaribu mbinu tofauti,” mbunge huyo alisema.

Aliongeza kuwa wataendelea kushirikiana na serikali na kupendekeza suluhisho kwa changamoto kama vile Mpango wa Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA), ufisadi, na masuala makuu ya sera.Musili anasema katika umri wake, Raila hana cha kupoteza akiacha maandamano ambayo ametumia kwa miaka mingi kupigania mabadiliko nchini.

“Nafikiri ndio sababu huwa anajitenga na washirika wake katika upinzani kufanya handisheki na viongozi wa serikali alivyofanya 2018 na Rais Uhuru Kenyatta na alivyofanya sasa na Rais Ruto,” asema.

Kwa Raila kuacha mapambano makali kupitia maandamano, wadadisi wanasema ni kufungua ukurasa mpya katika siasa za Kenya.

“ Kizazi kipya kinachipuka kuendeleza harakati ilivyoshuhudiwa mwaka jana vijana walipoandaa maandamano makubwa nchini na kuzima Sheria ya Fedha 2024. Hata Raila akiacha maandamano haimaanishi mwisho wa kukosoa serikali,” akasema Musili.