Raila aibuka kuwa mwokozi wa mahasimu wake
RAIS William Ruto yuko katika hali ambayo mtangulizi wake Uhuru Kenyatta alijipata mwaka wa 2018 hadi akamhitaji Bw Raila Odinga kwa dharura kuokoa serikali yake iliyokumbwa na upinzani mkali.
Kufikia wakati Bw Kenyatta alimkimbilia Bw Odinga kuomba usaidizi, alikuwa amebanwa na naibu wake, Dkt Ruto mwenyewe, ambaye alionekana kuwa tishio kwa utawala wake.
Badala ya kujaribu kumtimua Dkt Ruto, Bw Kenyatta alimtenga na akamtumia Bw Odinga kupata utulivu. Huku akijua vyema kwamba Bw Ruto angetumia idadi kubwa ya wabunge waliomuunga mkono kuyumbisha utawala wake, Bw Kenyatta alimwendea Bw Odinga na kuwa mwokozi wake kisiasa.
Walitia muhuri uhusiano wao kupitia handisheki ya Machi 9, 2018 na hivyo Bw Kenyatta akapata utulivu. Miaka saba baadaye, Dkt Ruto amekuwa rais na kujipata katika hali aliyomsababishia Kenyatta kwa kutofautiana na aliyekuwa naibu wake, Rigathi Gachagua, lakini akapanga upesi kumuondoa afisini kupitia bunge.
Labda katika kujaribu kufanya mambo kwa njia tofauti, badala ya kumvumilia Bw Gachagua kama vile Bw Kenyatta alivyomfanyia, Dkt Ruto alihakikisha Gachagua aliondolewa mamlakani. Kuna uwezekano kwamba kwa kufanya hivyo, Rais Ruto alifikiri angemaliza changamoto ya kutofautiana na naibu wake.
Alimchagua Prof Kithure Kindiki kutoka Mlima Kenya kuwa naibu wake.
“Lakini mambo yalikuwa tofauti sana ambapo kuchaguliwa kwa Bw Kindiki kulifanya eneo la Mlima Kenya kumfuata Bw Gachagua,” asema mchanganuzi wa siasa, John Okumu.
Bw Okumu anasema kuwa Rais Kenyatta alijua kwamba utawala wake ulitokana na kuungwa mkono na Bw Ruto hivyo basi aliepuka kumtimua kwa hofu ya kuanika udhaifu wake.
“Hili ndilo jambo ambalo Rais Ruto hakuzingatia katika mradi wake wa kumtimua Gachagua. Alizingatia tu idadi ya Mlima Kenya katika Bunge la Kitaifa na Seneti lakini hakuzingatia uwezekano wa wapiga kura wa eneo hilo kumkaidi,” Bw Okumu asema.
Aliamini kwamba Bw Kindiki angenyakua Mlima Kenya kwa haraka na kuuongoza kuendelea kumpenda Bw Ruto, lakini wapiga kura wa eneo hilo wameendelea kuasi, wakiambatana na Bw Gachagua ambaye amewaamuru kuvunja uhusiano na serikali na kutishia azma ya Bw Ruto kuchaguliwa tena 2027.
Wasiwasi wa Bw Kenyatta ulikuwa jinsi ya kudumisha ajenda yake baada ya mzozo wake na Bw Ruto.
“Ni katika kudumisha hali hiyo ambapo Bw Kenyatta alienda kwa Bw Odinga kuokoa serikali yake. Lakini katika hali ya kutatanisha ya Rais Ruto, wasiwasi wake mkubwa si nguvu ya kutunga sheria kwa vile anayo. Yake ni kuhusu kuchaguliwa tena 2027,” asema mchanganuzi wa kisiasa Prof Macharia Munene.

Prof Munene anasema kuwa “kosa kubwa zaidi alilofanya Rais Ruto ni kucheza kamari na idadi ya wafuasi wake akiwa bado katika muhula wake wa kwanza”.
Anasema kwamba “ikiwa Bw Kenyatta angevuruga idadi ya wafuasi wake katika muhula wa kwanza, angepoteza azma ya kuchaguliwa tena 2017, hali ambayo huenda ikampata Rais Ruto 2027”.
Anasema kuwa iwapo Bw Kenyatta angemtimua Dkt Ruto katika muhula wao wa kwanza afisini, Bw Odinga angechukua fursa hiyo kuungana na waliotimuliwa na kumng’oa mamlakani 2017.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT) Bw Charles Mwangi anasema kuwa ‘vivyo hivyo, Bw Kenyatta alilazimika kumwendea Bw Odinga kujikinga na Ruto, ndivyo Rais Ruto anaonekana kufanya kwa kusuka muungano na Bw Odinga.
Hii ni baada ya mpango wa awali wa Bw Odinga kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika (AUC) kugonga mwamba, ambapo kama angefaulu, Rais Ruto angerithi kura za Odinga ili kuwa na uhakika wa kuchaguliwa tena.
“Sasa hapa ndipo inapopendeza: Bw Kenyatta alijitokeza kumpiga vita naibu wake katika muhula wa pili, Rais Ruto amefanya hivyo katika muhula wa kwanza. Bw Kenyatta hakuwa na cha kupoteza lakini Rais Ruto ana kila kitu cha kupoteza,” akasema.