‘System ya Majambazi’: Sakata ya mawakili feki na machifu kupora watu mali yafichuka
CHAMA cha Mawakili Nchini (LSK) na wapelelezi kutoka Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) wamefichua njama ya kundi moja la walaghai wanaowapora maelfu ya watu pesa na mali, Nyahururu.
Wapelelezi wanasema kuwa genge hilo linashirikisha mawakili feki, machifu na maafisa wa Wizara ya Ardhi.
Kwa mujibu wa stakabadhi na faili zilizopatikana wakati wa operesheni katika afisi za kundi hilo la walaghai mjini Nyahururu, watu kadhaa kutoka Kaunti za Laikipia, Nyandarua, Baringo na Samburu wamelaghaiwa na mawakili hao feki wanaoshirikiana na maafisa wa serikali waliopotoka kimaadili.
Wakati wa operesheni iliyoendeshwa mwishoni mwa wiki, maafisa wa LSK na wale wa DCI waliwanasa washukiwa wawili, mwanamume na mwanamke, wanaojifanya kuendesha kampuni za mawakili wanaohudumu katika Kaunti za Kiambu na Nairobi.
Afisi hizo mbili ziko mita chache kutoka jengo la Mahakama ya Nyahururu na karibu na afisi za Wizara ya Ardhi.
“Inadaiwa kuwa wawili hao ni wanachama wa LSK lakini wanaendesha afisi hizo kwa kutumia majina yao. Aidha, majina yao hayako kwenye sajili ya mawakili nchini,” akasema Stephen Mbugua, wakili kutoka Afisa za LSK, Nairobi aliyesimamia operesheni hiyo akisaidiwa na mwenyekiti wa LSK tawi la Laikipia, Maureen Wanjiru.
“Shughuli zinazoendeshwa katika afisi hizi zinajumuisha kutiwa muhuri na saini kwa stakabadhi za mahakama,” Bw Mbugua akaongeza.
Afisa huyo wa LSK, Nairobi, pia alifichua kuwa mawakili ambao majina yao yalitumika kwenye vibao vilivyoko kando ya afisi hizo hawajatimiza kwa ukamilifu kanuni za chama hicho cha mawakili nchini.
Wapelelezi walipata muhuri wa mawakili walioko miji mingine kama vile Nyeri, pamoja na stakabadhi zilizotayarishwa kinyume cha sheria na walaghai hao.
LSK ilivutiwa na malalamishi kutoka kwa watu ambao wamepoteza pesa na mali kupitia shughuli zinazoendeshwa na mawikili hao feki wakishirikiana na machifu na maafisa wa Wizara ya Ardhi.
“Tumebaini kuwa mawakili hawana habari na hawajakubali kwamba mihuri yao itumike. Tumeendeleza uchunguzi hadi kwa mawakili walioidhinishwa na LSK wanaoshukiwa kuhusika katika sakata hiyo ya kufanikisha shughuli haramu.
“Tunashangaa kuwa baadhi ya kampuni zinazomilikiwa na wanachama wa LSK zinaendesha shughuli zao kinyume cha sheria katika kaunti ya Laikipia, bila ufahamu wa asasi hiyo inayosimamia mawakili. Ni afisi kama hizo zinazofanikisha shughuli haramu,” akasema Bw Mbugua.
Alisema uchunguzi utaendelezwa hadi kwa maafisa wengine wa serikali wanaohusika na shughuli hizo zinazokiuka sheria.
“Walaghai hao wanaendesha shughuli za uuzaji, ununuzi na urithi wa ardhi,” Bw Mbugua akaeleza.