Ruto amsifu Chebukati kwa kumtangaza rais 2022
ALIYEKUWA mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati alizikwa Jumamosi katika mazishi yaliyoibua kumbukumbu za kura ya urais katika uchaguzi mkuu wa 2022.
Viongozi wa serikali wakiongozwa na Rais William Ruto walimtaja kama shujaa kwa msimamo wake usioyumba huku familia yake ikifichua masaibu iliyopitia.
Rais William Ruto alirejelea madai yake kuwa viongozi mashuhuri katika utawala wa mtangulizi wake Uhuru Kenyatta wangemnyang’anya ushindi wake katika uchaguzi wa 2022 iwapo Bw Chebukati angeogopa vitisho vya wakuu wa serikali ya Uhuru Kenyatta.
Akihutubu wakati wa mazishi ya Bw Chebukati katika kijiji cha Sabata kaunti ya Trans Nzoia, Dkt Ruto alimsifu Bw Bw Chebukati kwa kusimama imara na kumtangaza kama mshindi.
“Nataka niseme hapa tena wazi kuwa watu fulani maarufu na wakuu katika serikali walitumia nguvu kulazimisha Bw Chebukati kubadilisha ushindi wangu lakini alisimama imara kwa haki kama shujaa na kunipa ushindi wangu,” alisema Bw Ruto.
Bw Ruto alimtaja marehemu Chebukati kama mtu mwadilifu, aliyesimamia haki ambaye uamuzi wake ulinusuru nchi baada ya uchaguzi wa 2022.Kiongozi huyo alisifia watoto wa marehemu kwa kuiga mfano wa baba yao wa kuwa na maadili mema.
“Nimeona tabia njema ya watoto wa marehemu nitaendelea kusimama nanyi,” alisema Bw Ruto. Wakati huo huo Rais Ruto alirejelea mkataba kati ya serikali na ODM ambapo alisema mkataba huo haulengi uchaguzi wa 2027. Rais Ruto alisema lengo la muungano huo ni kudumisha umoja wa Kenya na walai si wa kugawana vyeo.
“Ushirikiano wetu haulengi 2027 bali ni kudumisha umoja wa nchi na kuwezesha Wakenya wote kupata maendeleo bila kuzingatia mirengo ya kisiasa,” aliongeza Rais Ruto.
Familia ya aliyekuwa mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati ilisema kuwa ilipitia wakati mgumu wakati wa kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi mkuu wa 2022. Mjane wa Chebukati, Mary Chebukati alifichua kuwa mumewe alitishiwa.
“Mume wangu alisimulia jinsi alivyowekewa bunduki usoni huku akitishiwa maisha kutokana na uchaguzi mkuu wa 2022. Hali ilikuwa ngumu zaidi ambapo ilibidi zaidi ya wachungaji 40 kupiga kambi katika nyumba yangu kutuombea kutokana na hali ngumu na vitisho kwa maisha ya mume wangu,” alisema Bi Chebukati.
Bi Chebukati ambaye alikashfu mitandao ya kijamii kwa kuua mume wake mara kadha kabla ya kifo chake, alielezea namna baadhi ya vyombo vya habari vilivyodunisha marehemu.
Bi Chebukati alisema ilibidi apigie simu Askofu David Oginde ili kupata uhakika iwapo mume wake alikuwa hai. Alisema kuwa alivuta pumzi pale alipopata hakikisho kutoka kwa askofu Oginde kuwa Bw Chebukati alikuwa salama.
“Kwa sababu Askofu Oginde ni mtumishi wa Mungu nilipata hakikisho mzee alikuwa salama na kufanya familia yangu ipumue,” alisema Bi Chebukati.
Vile vile Bi Chebukati alipongeza walinzi wa marehemu kwa kudumisha usalama wake wakati wa vurumai katika Bomas of Kenya. ‘Tunashukuru walinzi wa mzee wakati wa kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi mkuu wa 2022, walifanya kila juhudi kuhakikisha usalama wa mume wangu,” aliongeza Bi Chebukati.