Mbadi aomba minofu zaidi ya ofisi za Ruto, Kindiki na Mudavadi
HAZINA ya Kitaifa imewasilisha ombi la nyongeza ya Sh3.3 bilioni, ambazo sehemu kubwa ya fedha hizo zitatumika katika Ikulu, Ofisi ya Mkuu wa Mawaziri, Naibu wa Rais na Huduma za Afya.
Kulingana na ripoti ya Kamati ya Uratibu kuhusu Makadirio ya Bajeti ya Pili ya Ziada kwa mwaka wa kifedha unaoisha Juni 2025, Idara ya Huduma za Matibabu imeomba nyongeza ya Sh2 bilioni.
Ikulu imeomba Sh400 milioni za ukarabati, huku Ofisi ya Mkuu wa Mawaziri, inayoongozwa na Musalia Mudavadi, ikiomba Sh100 milioni zaidi kwa shughuli zake na ukarabati.
“Hazina ya Kitaifa ilisema pamoja na maombi yaliyopo katika bajeti ya nyongeza ya mwaka wa kifedha wa 2024/25, imepokea maombi mengine ya nyongeza ya Sh3.3 bilioni kufanikisha vipaumbele vipya na imeomba Kamati kuzingatia hilo,” ilisema kamati hiyo inayoongozwa na Naibu Spika Gladys Shollei.
Kamati hiyo ilipunguza matumizi ya hivi majuzi ya Ikulu kwa Sh150 milioni kabla ya kuidhinisha ombi lake jipya la Sh400 milioni, na hivyo kuongeza bajeti yake hadi Sh4.05 bilioni.
Hii inafanya bajeti ya jumla ya Ikulu kufika Sh4.2 bilioni, awali ikiwa Sh3.8 bilioni katika bajeti ya mwaka wa kifedha unaoisha Juni 2025.
Ombi la Bw Mudavadi la Sh100 milioni lilihusu gharama za uendeshaji na matengenezo, ambapo kamati iliidhinisha kiasi hicho na mapendekezo hayo yatawasilishwa kwa Bunge la Kitaifa kujadiliwa na kupitishwa kabla ya kuwasilishwa kwa Rais William Ruto.
Idara ya Barabara iliomba nyongeza ya Sh200 milioni, Bunge la Kitaifa (Sh120 milioni), Usalama wa Ndani (Sh159 milioni), na Huduma za Magereza (Sh100 milioni), huku Hazina ya Kitaifa na Wizara ya Biashara kila moja ikiomba Sh50 milioni.
Katika bajeti ya nyongeza, Ikulu, Ofisi za Naibu Rais Prof Kithure Kindiki na Bw Mudavadi zilitengewa Sh5 bilioni zaidi kwa mishahara, safari, na burudani, licha ya serikali kupunguza matumizi yasiyo ya lazima.
Bajeti ya Ikulu inajumuisha matumizi yasiyoelezwa ya Sh1.5 bilioni, Sh732.2 milioni za safari za ndani, Sh700 milioni za mishahara na marupurupu, na Sh312.4 milioni za matengenezo ya magari.
Ofisi ya Prof Kindiki, ambayo haikuomba nyongeza, ilitengewa Sh420.4 milioni zaidi kwa mishahara na safari, huku ofisi ya Bw Mudavadi ikitengewa Sh133.4 milioni zaidi.
Ombi hili la bajeti ya matumizi ya kawaida linajiri wakati serikali inasisitiza kupunguza gharama za matumizi yasiyo ya lazima kama safari na burudani ili kupunguza uhaba wa fedha unaosababishwa na nakisi katika ukusanyaji ushuru.