Waumini wa Kanisa Katoliki wamwombea Papa Francis
BUENOS AIRES, Argentina
MAELFU ya raia wa Argentina, wengi wao kutoka vitongoji duni vya jiji kuu, walikongamana katika kanisa moja viungani mwa Buenos Aires kumwombea Papa Francis, ambaye amelazwa kwa zaidi ya mwezi mmoja.
Wakiwa wamebeba magoma, vijibendera na mikebe ya maji takatifu, waumini wa Kanisa Katoliki na makasisi walijumuika pamoja katika Kanisa la Gothic Basilica of Our Lady of Lujan, kumtakia Papa huyo afueni anapoendelea kutibiwa maradhi ya kupumua.
“Maisha marefu kwa Papa Francis!” Kasisi Jose Maria ‘Pepe’ di Paola, mwanachama wa kundi moja la makasisi katika vitongoji duni, akawaambia waumini.
“Hivi ndivyo tunapaswa kuwa kama Kanisa, anavyotufunza Papa Francis, kanisa linalojali masilahi ya watu masikini.”
Papa Francis ni raia wa Argentina na mtu wa kwanza kutoka eneo la Latin Amerika kushikilia wadhifa huo.
Ripoti ya hivi punde kutoka Vatican, kuhusu hali ya afya ya Papa Francis, inasema kuwa hali yake inaendelea kuimarika.
Lakini hospitali ya Gemelli, iliyoko jijini Roma, alikolazwa haijasema ni lini ataruhusiwa kuondoka.