Habari za Kaunti

Hofu wakulima wakiacha kilimo cha nazi

Na KALUME KAZUNGU March 17th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

WAKULIMA wa nazi kisiwani Lamu wameeleza hofu ya kilimo hicho kusambaratika siku za usoni kutokana na upungufu wa mazao.

Nazi nyingi ambazo huuzwa kisiwani Lamu hutoka maeneo ya Makafuni, Bombay, Shella na Matondoni.

Siku za hivi karibuni, kiwango cha nazi katika soko la Manispaa ya Lamu kimepungua, hali inayotajwa kuchangiwa na idadi ndogo ya wakulima.

Bw Abdulrahman Mohamed, mkulima wa nazi mtaani Bombay, alisema wengi wao walikata minazi ya mbegu za zamani kisha hawakupanda mingine mipya.

“Hakuna motisha tena ya kilimo cha nazi. Tunategemea soko la rejareja ambalo haliingizi faida. Ndiyo sababu wengi wetu tumekata minazi na kuelekeza nguvu zetu kwa sekta nyingine kama vile uvuvi,” akasema Bw Mohamed.

Bw Ali Sahe, muuzaji nazi katika soko la Manispaa ya Lamu, alikiri kukumbwa na upungufu wa bidhaa hiyo.

“Zamani ilikuwa rahisi kwangu kununua nazi na kuuza hapa sokoni. Nazi nyingi zilitoka Matondoni, Makafuni na kwingineko. Leo hii hali ni tofauti. Kuna uhaba wa nazi kisiwani,” akasema Bw Sahe.

Wachuuzi wengine walikiri kulazimika kununua nazi kutoka nje ya Lamu, ikiwemo Siyu, Pate, Bahari na Hongwe, ambapo wamepata ugumu wa kuzisafirisha hadi mjini Lamu kuuza.