Habari Mseto

Ajenti wa kuuza mashamba alia LSK kumpaka tope

Na RICHARD MUNGUTI March 18th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

AJENTI wa kuuza mashamba na nyumba anayeshirikiana na kampuni ya mawakili katika kesi zake ameshtaki chama cha wanasheria nchini (LSK) kwa kumchafulia jina.

Ajenti huyo anaomba mahakama kuu iamuru LSK kumlipa fidia kwa kumpaka tope na wakati huohuo izimwe kueneza habari za uongo kumhusu.

Bw Stephen Mwangi Kimani, ambaye pia ni mkurugenzi wa kampuni ya Eldolim Properties Limited anaomba mahakama kuu ishurutishe LSK imlipe fidia kwa kuchapisha katika mtandao wa Facebook kwamba anajifanya kuwa wakili.

Bw Kimani alimweleza Jaji Stellah Mutuku katika kesi aliyoshtaki chini ya sheria za dharura kwamba LSK ikishirikiana na mpinzani wake wa kisiasa Bw Joseph Karanja Muchai wamemshushia hadhi yake.

Bw Kimani amedokeza kwamba alifika katika kituo cha polisi cha Limuru ambapo aliagizwa afike na mawakili wanaohudumu katika eneo la Limuru na kuhojiwa.

Wanachama wa LSK walikuwa wamepiga ripoti kwamba Bw Kimani anajitambua kama wakili kwa wateja.

“Baada ya kuhojiwa na maafisa wa polisi kituo cha polisi cha Limuru suala hilo lilisuluhishwa. Tukiwa mle kituo wawakilishi wa LSK walinipiga picha ambazo zimetumika bila idhini yangu kusambazwa katika mitandao ya kijamii,” anasema Bw Kimani katika ushahidi aliowasilisha mahakama kuu.

Mlalamishi huyu anaomba mahakama izime LSK na Bw Muchai kusambaza habari za uongo kwamba “yeye (Kimani) anajifanya wakili.”

Mlalamishi anaeleza mahakama kwamba sifa zake zimedunishwa na kwamba azma yake ya kuwania ubunge wa Limuru 2027 unazoroteshwa na habari hizo zinazosambazwa na Bw Muchai ambaye ni mpinzani wake kisiasa.

Jaji Mutuku alielezwa kwamba Bw Muchai anasimamia mtandao ulio na wasomaji zaidi ya 70,000 ambapo anapeperusha habari hizo za uongo.

Anaomba mahakama iamuru alipwe fidia na LSK na Bw Muchai kwa kumharibia sifa.