Hakimu aonya polisi dhidi ya kunyoa washukiwa bila idhini yao
HAKIMU mmoja mjini Eldoret amewaonya polisi dhidi ya kunyoa nywele za washukiwa bila ridhaa yao.
Hakimu mwandamizi Caroline Watimah alisema kitendo hicho ni sawa na mateso na ukiukaji wa haki za kimsingi za binadamu.
Bi Watimah alikuwa akirejelea kisa ambapo mvulana mwenye umri wa miaka 16 alidaiwa kunyolewa akiwa mikononi mwa polisi kabla ya kufikishwa kortini.
Mvulana huyo alimwambia hakimu kwamba polisi walimnyoa bila idhini yake.
“Kwa kunyoa mvulana aliye chini ya ulinzi wa polisi ni kumuathiri kisaikolojia. Tayari ana woga hata tunapozungumza naye sasa. Hii tabia si nzuri,” alisema Bi Watimah huku akishauri maafisa kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) kuwaelimisha polisi kuhusu hatari ya kunyoa nywele za mshukiwa bila idhini yao.
Mvulana huyo alishtakiwa kwa kuiba vifaa vya kielektroniki mnamo Machi 17 katika mtaa wa Kipkaren katika Kaunti-ndogo ya Kapseret, mali ya Samuel Makokha yenye thamani ya Sh13,000.
Hata hivyo, hakuruhusiwa kujibu mashtaka akisubiri umri wake kuthibitishwa.
Bi Watimah ambaye pia ni naibu msajili wa mahakama ya Eldoret aliagiza polisi kuhakikisha mshukiwa anashughulikiwa kama mtoto anayehitaji matunzo na ulinzi kwa kuzuiliwa katika seli ya mtoto akisubiri kutathminiwa umri kabla ya kufunguliwa mashtaka.
Aliagiza kesi hiyo itajwe Machi 19.