Sakaja akivutia watoto shuleni kwa chapati, mwenzake wa Nyamira anatumia uji
SERIKALI ya Kaunti ya Nyamira imetangaza mpango wa kutoa lishe ya uji kwa wanafunzi wa chekechea walioko katika shule za umma.
Gavana wa kaunti hiyo Amos Nyaribo, amesema mpango huo utaanza kutekelezwa kuanzia muhula ujao.
Kulingana na Bw Nyaribo, mpango huo utakuwa na madhumuni ya kuongeza idadi ya wanafunzi katika shule za umma.
Kulingana na kiongozi huyo wa chama cha United Progressive Alliance (UPA), hatua hiyo pia itasaidia kutoa lishe bora kwa wanafunzi wanaotoka katika jamii maskini.
“Serikali yangu imeweka pesa kuanzia muhula ujao ili kupeana kikombe cha uji wenye virutubisho kamili kwa wanafunzi wa chekechea. Tumegundua kuwa familia nyingi hazina chakula cha lishe bora kwa wanao ambao ni wanafunzi. Ndio maana tumechukua hatua hiyo ya kuwalisha wanafunzi wetu zaidi ya 30,000 na uji,” gavana huyo alisema mnamo Jumatatu, Machi 17, 2025 alipoongoza hafla ya siku ya elimu ya kaunti hiyo katika eneo la Manga.
Katika hafla hiyo, gavana Nyaribo alisema serikali yake itazidi kuinua viwango vya elimu ya chekechea katika gatuzi la Nyamira kwa kuendeleza ujenzi wa madarasa mapya.
Gavana Nyaribo alisema serikali yake itazidi kupiga jeki elimu ya vyuo anuwai na akawasihi vijana kujiunga na taasisi hizo kwa kozi za kiufundi alizosema kwa sasa ndizo zinazozalisha ajira nyingi.
Mbunge wa Kitutu Masaba Clive Gisairo ni miongoni mwa viongozi waliohudhuria hafla hiyo ya kuwazawadi wanafunzi na shule zilizotia fora katika mitihani ya kitaifa ya mwaka uliopita, 2024.
Mbunge huyo wa awamu ya kwanza alisema watazidi kupigania maslahi ya walimu, hasa wale walio kwenye kandarasi ili kuimarisha viwango vya elimu nchini.
Mpango wa Gavana Nyaribo, unaonekana kuwiana na mwenzake wa Nairobi, Johnson Sakaja ambaye ana mpango wa chapati kuvutia wanafunzi katika shule za umma.
Siku kadha zilizopita, Rais William Ruto alimtaka Bw Sakaja kutafuta mashine yenye uwezo wa kupika chapati 1, 000, 000 akiahidi kumnunulia.