Zaidi ya watu 2 milioni kaunti 23 wanahitaji msaada wa chakula – ripoti
KUPUNGUA kwa mvua ya vuli mwaka jana, 2024, kulisababisha kuongezeka kwa idadi ya watu wanaohitaji msaada wa kibinadamu na ongezeko la visa vya watoto na wanawake wajawazito wanaohitaji matibabu kwa utapiamlo mkali.
Hii ni kwa mujibu wa ripoti ya Mamlaka ya Kitaifa ya Usimamizi wa Ukame (NDMA).
Ripoti hii inafuatia tathmini iliyofanywa katika kaunti 23 zinazotambuliwa kama maeneo kame na nusu-kame (ASAL) kati ya Januari 20 na Februari 18, 2025, na Kundi la Kusimamia Usalama wa Chakula Kenya, ambalo linaleta pamoja mashirika yanayojumuisha idara za serikali, mashirika ya Umoja wa Mataifa, na yasiyo ya kiserikali.
Ripoti hiyo, yenye kichwa ‘Tathmini ya Usalama wa Chakula na Lishe kuhusiana na Mvua ya vuli 2024,’ inaonyesha kuwa watu 2.15 milioni katika kaunti za ASAL wanahitaji msaada wa kibinadamu kwa dharura, idadi hii ikiwa imeongezeka kutoka milioni moja iliyorekodiwa Julai 2024.
Kaunti zilizoathirika zaidi ni Turkana, Mandera, Garissa, Wajir, na Marsabit.
“Idadi ya watoto (wenye umri wa miezi sita hadi 59) wanaohitaji matibabu ya utapiamlo mkali iliongezeka kutoka 760,488 hadi 800,202, huku visa vya wanawake wajawazito na wanaonyonyesha vikiongezeka kutoka 112,401 hadi 120,732, hali inayoashiria kudorora kwa lishe hasa katika maeneo kame na kavu na ongezeko la hatari kwa makundi haya mawili,” inasema ripoti hiyo.
Ripoti hiyo ilitaja sababu kuu za ukosefu wa chakula kuwa ni mvua ya vuli ya 2024 ambayo haikufikia wastani, mafuriko yaliyosababisha watu kuhama, bei ya juu ya bidhaa, uzalishaji duni wa mazao, magonjwa ya binadamu na mifugo, wadudu wanaoharibu mazao, na migogoro ya kiusalama.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, maeneo 17 yanakabiliwa na hatari ya ukosefu wa chakula kwa dharura mwezi huu, Machi.
Maeneo haya ni Pokot Magharibi, Samburu, Isiolo, Meru, Laikipia, Baringo, Nyeri, Tharaka, Mbeere, Koibatek, Kitui, Tana River, Kajiado, Makueni, Kilifi, Kwale, na Lamu.
Hatua ya ukosefu wa chakula kwa dharura, kulingana na Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP), inamaanisha familia zinaweza kuwa na kiwango cha chini cha chakula kinachokidhi mahitaji yao lakini zinakumbwa na changamoto za kumudu mahitaji mengine muhimu ya kimsingi.
“Hawa ni watu ambao wana mapato yasiyo ya uhakika, wanakabiliwa na ugumu wa kukidhi mahitaji yao ya msingi na wanapaswa kufanya mabadiliko ili kusaidia mahitaji yao yasiyo ya chakula. Katika hatua hii, kati ya asilimia tano na 10 ya watu wanakabiliwa na utapiamlo mkali, na mtu mmoja anapata kalori 2,100 kwa siku, kiasi kinachomaanisha kuwa chakula wanachopata hakitoshi kikamilifu kukidhi mahitaji yao ya lishe,” inasema WFP.
Kaunti za Turkana, Marsabit, Mandera, Wajir, na Garissa ziko kwenye hatua ya kuhitaji chakula kwa dharura.
Katika hatua hii, familia zinakabiliwa na upungufu mkubwa wa chakula na utapiamlo mkali au zinaweza tu kukidhi mahitaji yao ya chakula kwa kutegemea misaada ya dharura.