Wakenya walia SHA na ushuru wakikutana na timu ya Omtatah
KAMATI ya kuchunguza ufaafu wa Urais wa seneta wa Busia, Okiya Omtatah, imezuru karibu nusu ya nchi katika harakati zake za kukusanya maoni kutoka kwa Wakenya kuhusu masuala yanayopaswa kushughulikiwa na serikali.
Kamati hiyo imebaini kuwa Wakenya wengi wana wasiwasi kuhusu sera ya ushuru, ambapo wafanyabiashara wanalalamikia viwango vya juu vya kodi.
Wafanyabiashara wanalalamika kuwa ushuru unaotozwa na serikali za kaunti na serikali kuu unawafanya washindwe kuendesha biashara zao, huku baadhi yao wakilazimika kufunga biashara.
Wengine pia wameeleza changamoto wanazokumbana nazo katika kupata huduma za afya wanapotumia Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA).
Wanafunzi wa vyuo vikuu pamoja na wazazi wao wameeleza wasiwasi kuhusu mfumo mpya wa ufadhili wa elimu ya juu, ambapo wanafunzi hupangwa katika makundi tofauti kulingana na hali ya kiuchumi ya familia zao.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mary Kathomi, Wakenya wengi wanakabiliwa na changamoto zinazofanana, huku masuala yaliyoorodheshwa hapo juu yakitajwa mara nyingi zaidi.
“Vijana wanahofia ukosefu wa ajira na wanataka kufahamu jinsi wanavyoweza kuchangia ukuaji wa uchumi kupitia uundwaji wa nafasi za kazi,” alisema.
Aidha, alisema kuna maeneo fulani ambako wananchi wanakabiliwa na matatizo yanayofanana.
“Maeneo ambako matatizo sawa yanakumba kaunti nyingi ni yale yanayohusu kilimo. Wakulima wa kahawa katika maeneo mbalimbali wanakumbwa na matatizo sawa ambayo wangependa serikali iyashughulikie,” alisema Bi Kathomi.
Kamati hiyo ilitembelea Kaunti ya Homa Bay Jumanne, Machi 18, 2025 ambapo ilikutana na wakazi na kujadili masuala tofauti.
Bi Kathomi alisema kuwa timu yake imetembelea kaunti 18 hadi sasa katika juhudi zao za kukusanya maoni ya Wakenya.
Maoni haya yanatarajiwa kumsaidia Seneta Omtatah kuandaa sera na manifesto yake kwa uchaguzi wa urais mwaka 2027.
“Tunawapa Wakenya fursa ya kueleza masuala yanayowahusu, ambayo yatakuwa sehemu ya manifesto ya Okiya Omtatah,” alisema mwenyekiti huyo wa kamati.
Alisema kuwa mazungumzo na wananchi yataendelea kwa muda wa miezi mitatu ijayo.
Katika mikutano hiyo, baadhi ya Wakenya walitoa mapendekezo ya kutatua matatizo yanayowakumba.
Mwanachama wa Kamati hiyo, Dancan Onyango, alisema baadhi ya wananchi wanapendekeza kuwa serikali iunganishe mipango yote ya basari na kuzitumia kusaidia wanafunzi wanaotoka katika familia maskini.
“Maoni haya yatamsaidia Seneta Omtatah kuandaa mipango na sera zitakazomwezesha kuomba kura kwa msingi wa mahitaji ya Wakenya. Kila kaunti ina changamoto zake za kipekee, lakini baadhi ni sawa katika maeneo mengi,” alisema Onyango.