Habari za Kitaifa

Mandera kifua mbele, Sakaja akivuta mkia kwenye utekelezaji maendeleo

Na MARY WANGARI March 19th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KAUNTI ya Mandera inaongoza orodha ya tano bora huku Nairobi ikiwa miongoni mwa kaunti zinazovuta mkia katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, imesema ripoti mpya ya Mdhibiti wa Bajeti (CoG), Margaret Nyakang’o.

Mandera inayoongozwa na Gavana Mohamed Adan Khalif iliandikisha kiwango cha juu zaidi cha matumizi ya bajeti ya maendeleo kwa asilimia 32 katika kipindi cha miezi sita ya kwanza kwenye bajeti ya 2024/2025.

Ripoti mpya ya CoG inayoangazia nusu ya kwanza ya mwaka wa kifedha kati ya Julai na Desemba 2025, inaashiria kuwa Mandera ilipokea Sh14.89 bilioni zilizojumuisha fedha za kufadhili maendeleo Sh5.94 bilioni (asilimia 40) na matumizi mengineyo Sh8.95 bilioni (asilimia 60).

Narok (asilimia 30) Garissa (asilimia 28), Uasin Gishu (asilimia 27) na Marsabit (asilimia 26) zinafunga orodha ya kaunti tano bora zilizoandikisha matokeo bora katika utekelezaji wa bajeti ya maendeleo.

Kaunti nyinginezo zilizoandikisha matokeo bora kuhusiana na maendeleo katika kipindi hicho ni pamoja na Nandi na Machakos asilimia 25 mtawalia, Kwale (asilimia 24) Busia (asilimia 23) na Kericho (asilimia 22), zilifunga orodha ya 10 bora katika utekelezaji wa bajeti ya maendeleo, ilisema ripoti hiyo.

Jiji kuu la Nairobi ni miongoni mwa kaunti zilizoandikisha kiwango cha chini zaidi cha utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa asilimia sita.

Tana River na Baringo, asilimia saba mtawalia, Nyeri, Kisumu, na Taita Taveta (asilimia sita kila moja) Elgeyo Marakwet, Kitui, Lamu, Nakuru (asilimia tano kila moja), Kisii na Nyamira, asilimia nane kila moja ni kaunti 12 zilizoandikisha matokeo duni kimaendeleo.

Kifungu 107(2)(b) cha Sheria kuhusu Usimamizi wa Fedha za Umma (PFM) 2012 kinaagiza serikali za kaunti kutenga kiasi kisichopungua asilimia 30 ya bajeti kufadhili miradi ya maendeleo.

Sheria inasisitiza vilevile umuhimu wa kuhakikisha fedha hizo zinatumika kikamilifu.

Mdhibiti Bajeti alisema, “Katika kipindi hicho, serikali za kaunti zilitumia Sh33.60 bilioni kwa shughuli za maendeleo kiasi kinachoashiria asilimia 16 tu dhidi ya bajeti ya mwaka mzima kuhusu maendeleo ya Sh211.53 bilioni.”

Kwa jumla, kaunti 12 miongoni mwa kaunti zote 47 ziliandikisha chini ya asilimia 10 kuhusiana na utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika maeneo husika.

Katika mapendekezo yake, Bi Nyakan’go amesema serikali za kaunti ni sharti zipatie kipaumbele shughuli za maendeleo ili kutimiza matakwa ya sheria yanayoagiza kutenga asilimia 30 ya bajeti kwa shughuli za maendeleo, inavyoelezwa katika Sheria ya PFM 2012.

“Mikakati thabiti ya mipangilio, uangalizi na utekelezaji inapaswa kubuniwa kuimarisha kiwango cha matumizi ya fedha za maendeleo na kuimarisha maendeleo ya nchi.”