Naibu Gavana Kiambu ashtakiwa kwa kuzuia mwili wa babake uzikwe
NAIBU Gavana Kiambu Rosemary Njeri Kirika ameshtakiwa pamoja na watu wengine katika mzozo wa mazishi kuhusu baba yake Mzee James Kinani Mburu.
Mzee Mburu aliaga Novemba 20, 2024 na mwili wake umehifadhiwa katika chumba cha maiti cha Hospitali ya Misheni ya Kijabe.
Katika mzozo, huo watoto wa mke wa kwanza wa Mzee Mburu wanaomba mahakama iamuru baba yao azikwe kulingana na sheria na desturi za jamii ya Agikuyu.
Kulingana na sheria na desturi za jamii hii ya Agikuyu mwanamume akiwa na wake zaidi ya mmoja akiaga huzikwa katika boma ya mke wa kwanza.
Pia, sheria hizi zinasema mwanamume kifungua mimba ndiye huonyesha mahali baba yake atakapozikwa.
Katika kesi iliyoshtakiwa na mawakili Stanley Kinyanjui na Danstan Omari, watoto wa Phelis Wanjiku Mburu – (mke wa kwanza wa Mzee Mburu) aliyeaga wanaomba baba yao azikwe Gatanga kaunti ya Murang’a.
Lakini Naibu Gavana wa Kiambu – Rosemary Njeri Kirika pamoja na washtakiwa wengine wanaomba azikwe Gilgil kaunti ya Nakuru.
Walalamishi katika kesi hii – Ides Wairimu Mburu, Joyce Muthoni Mburu, Hannah Wanjiku Mburu na Antony Kinani Mburu wamewashtaki Charles Vincent Waweru, Rosemary Njeri Kirika, Alice Wambui, Geoffrey Ng’ang’a, Regina Muthoni na Patricia Karanja.
Katika kesi hiyo, hakimu Gerald Gitonga ameelezwa na walalamishi kwamba washtakiwa wanataka kuwafuja urithi wao kwa kutaka marehemu azikwe Gilgil.
Bw Gitonga alifahamishwa Mzee Mburu aliaga Novemba 20, 2024 na mwili wake umehifadhiwa katika chumba cha maiti hospitali ya Kijabe.
Novemba 25, 2024, hakimu alielezwa washtakiwa walifika katika hospitali hiyo wakidai mwili wa Mzee Mburu wakauzike lakini wakanyimwa kufuatia agizo la mahakama.
Mzee Mburu aliaga akiwa na umri wa miaka 90.
Mashahidi waliofika mbele ya Gitonga walisema kwamba Mzee wa rika ya Mburu huzikwa kwa mujibu wa sheria, desturi na tamaduni za Agikuyu.
Walalamishi wamepuuzilia mbali uamuzi na mapendekezo ya kamati ya wazee iliyokutana Desemba 2024 bila kuwashirikisha familia iliyopitisha Mzee Mburu azikwe Gilgil.
Kesi inaendelea.