Habari za Kitaifa

Wamuchomba: Vijana wanachangia ufanisi wa kilimo cha kahawa

Na WYCLIFFE NYABERI March 27th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MBUNGE wa Githunguri Gathoni Wamuchomba amewahimiza wakulima wa kahawa katika Kaunti ya Kisii kukumbatia mbinu za kidijitali ili kuimarisha ukuzaji wa zao hilo.

Kiongozi huyo alisema kuwa iwapo viwanda vingi vya kahawa Kisii vinataka kufufuka, vinapaswa kuwahusisha vijana katika masuala ya uongozi.

Akiongea mnamo Jumatano, Machi 26 katika kijiji cha Mokubo, eneobunge la Bomachoge Borabu, Kaunti ya Kisii, mbunge huyo alisema hizo ndizo sababu kuu zinazowaweka wakulima wa kahawa wa eneo la Mlima Kenya kifua mbele ikilinganishwa na wenzao kutoka maeneo mengine ya nchi.

Ziara ya Bi Wamuchomba ilijiri baada ya mbunge huyo kupokea mwaliko kutoka kwa serikali ya Kaunti ya Kisii, inayoongozwa na Gavana Simba Arati.

“Wapeni nafasi vijana ambao wamehitimu vyuo vikuu kushikilia baadhi ya nafasi katika uongozi wa viwanda na vikundi vyenu. Vijana hawa wana ujuzi mzuri wa kutumia mitandao. Wao ndio wanaoweza kuona bei nzuri wakati kahawa yenu inauzwa minadani,” Bi Wamuchomba alisema.

Mbunge huyo alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa serikali ya kitaifa kupiga jeki wakulima wa kahawa kwa kuyafuta madeni ambayo yamewakaba kwa miaka mingi.

“Serikali iliahidi wakulima wa kahawa mabilioni ya pesa lakini pesa hizo zote hazikutolewa. Leo hii ninasimama hapa Kisii kuiambia serikali iachilie pesa hizo ili kuwainua wakulima,” Bi Wamuchomba aliongeza.