Habari Mseto

Kaunti 21 zaitwa kusuluhisha zogo la wauguzi

February 6th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na PETER MBURU

KAMATI ya seneti kuhusu leba Jumatano iliamrisha serikali za kaunti 21 pamoja na Baraza la Magavana (CoG) kufika mbele yake Ijumaa, ili kufanya kikao na Muungano wa Kitaifa wa Wauguzi (KNUN) kwa lengo la kusitisha mgomo wa wafanyakazi hao, uliolemaza shughuli za afya katika kaunti 10 kwa siku tatu hadi sasa.

Hii ilikuwa baada ya viongozi wa wauguzi kufika mbele ya kamati Jumatano asubuhi na kuieleza namna serikali hizo pamoja na baraza la CoG zimekuwa zikiwazungusha ili kukwepa kuwalipa marupurupu ambayo walielewana tangu 2017.

Viongozi hao walieleza kamati hiyo kuwa japo mnamo Novemba 2, 2017 walitia saini mkataba na Baraza la Magavana ambalo lilikuwa likiwakilisha serikali za kaunti kuhusu marupurupu ya sare na huduma za ziada kwa wauguzi baada yao kushiriki mgomo mrefu, CoG sasa imekwepa jukumu na kudai kuwa si mwajiri wao.

Kutoka kushoto: Wanachama wa Kamati ya Seneti kuhusu Leba Maseneta Mutula Kilonzo Jr, Samson Cherargei na Johnston Sakaja waliposikiliza hali ya uuguzi nchini Februari 6, 2019. Picha/ Peter Mburu

Wakiongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa KNUN Maurice Opetu, viongozi hao walisema kuwa kaunti nyingi zimejitolea kulipa marupurupu hayo, japo baraza la CoG linavuta juhudi zao nyuma.

“Naamrisha kuwa Ijumaa hii saa nne asubuhi, sharti tuketi na muungano wa wauguzi, baraza la CoG, wizara ya Fedha, Tume ya Uratibu wa Mishahara (SRC) na Wizara ya Afya. Wote sharti waje ili tutatue suala la mgomo huu,” mwenyekiti wa kamati hiyo Johnston Sakaja akasema.

Vilevile, aliamrisha kaunti za West Pokot, Kisumu, Kisii, Taita Taveta, Trans Nzoia, Elgeyo Marakwet, Wajir, Homa Bay, Marsabit, Nyeri, Garissa, Kirinyaga, Embu, Muranga, Busia, Nakuru, Narok, Nandi, Bomet, Tana River, Samburu na Siaya kufika mbele ya kamati hiyo kesho, ili zieleze kwanini hazijalipa pesa hizo.

Seneta Mutula Kilonzo na Johnson Sakaja wakikagua stakabadhi za wauguzi. Picha/ Peter Mburu

Kufikia jana, wauguzi katika kaunti 10 walikuwa wamesusia kazi kwa siku ya tatu, japo kaunti zingine zilijadiliana na wafanyakazi hao na kuelewana kusitisha mgomo.Katika kaunti ya Nairobi, Gavana Mike Sonko aliketi na wafanyakazi hao Jumanne hadi saa nne usiku hadi wakaelewana na wakasitisha mgomo baada ya kususia kazi siku mbili.

Makubaliano yao yalikuwa kuwa wauguzi wataanza kulipwa marupurupu hayo kuanzia kesho.Vilevile, kaunti za Mombasa, Migori na Machakos tayari zimeanza kuwalipa wauguzi wao na hivyo kazi inaendelea bila matatizo.

Katika kaunti zingine 14 zikihusisha; Baringo, Laikipia, Meru, Bungoma, Nyamira, Isoiolo, Kericho, Kakamega na Kilifi, wauguzi wamefanya maelewano na serikali za kaunti na kuahidiana wakati watalipwa na hivyo wakasitisha mgomo.

Majadiliano baina ya maseneta na wauguzi katika Jumba la Red Cross, Nairobi. Picha/ Peter Mburu

“Katika kaunti ambazo serikali zimekubali kuketi nasi na kufanya maelewano ya aina yoyote ile, aidha kwa kuandika, ama ya kawaida, wafanyakazi wetu wamesitisha mgomo na kuzipa muda.

Kaunti ambapo mgomo unashuhudiwa ni zile serikali hazikubali kuketi nasi ama zinatutuma katika idara zingine,” akasema Bw Opetu.Lakini wanachama wa kamati hiyo ya leba walieleza kughadhabishwa kwao na jinsi serikali za kaunti, Tume ya SRC na baraza la CoG zimekuwa zikiwazungusha wafanyakazi hao, wakisema lengo lao ni kuchelewesha haki.

“Hii haikubaliki, huu ni mchezo wa kuchelewesha kutekelezwa kwa maelewano na wauguzi. Wauguzi ni wafanyakazi wa umuhimu sana na hatuwezi kuruhusu hali hii kuendelea,” akasema seneta Sakaja.

Tayari kaunti za Garissa, Samburu, Kirinyaga na Embu zinasubiri kuanza mgomo wao mnamo Februari 11, nazo za Muranga, Busia, Nakuru na Siaya zikisubiri kususia kazi Februari 18.

Hali hii ya mgomo wa wauguzi imekuwa ikisababisha mahangaiko miongoni mwa maelfu ya Wakenya wanaotafuta huduma za afya, kwani ni wauguzi ambao huwahudumia wagonjwa wengi, hata kuliko madaktari.

Vilevile, kiwango cha pesa wanachodai wafanyakazi hao ni cha chini kwani katika kaunti nyingi, pesa za kugharamia malipo hayo kwa mwaka ni chini ya Sh30milioni kwa wauguzi wote.