Kaunti chonjo kisa kinachoshukiwa cha kipindupindu kikiripotiwa Nyando
MAAFISA wa Afya Kaunti ya Kisumu wameanza kujiandaa kupambana na ugonjwa wa kolera baada ya kisa kinachoshukiwa cha maradhi hayo kuripotiwa Kaunti ndogo ya Nyando.
Hii ni baada ya msichana mwenye umri wa miaka 14 kuaga dunia kutokana na maradhi yanayodaiwa kuwa ya kipindupindu. Kwa mujibu wa maafisa wa afya, mamake msichana huyo alikuwa amelazwa hospitalini mnamo Machi 13 kutokana na maradhi ambayo dalili zake zinakisiwa kuwa za kipindupindu.
Supritendanti wa Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Ahero Dkt Kevin Ochieng’ jana alisema kuwa kwa muda wa mwezi moja uliopita, wamekuwa wakitibu wagonjwa ambao wanaendesha hasa kutoka eneo la Onjiko.
“Wiki jana tuliwapokea wagonjwa watatu na hadi sasa watu wawili wamelazwa na kutibiwa. Wengine wanaendelea kupimwa na wanafuatiliwa na hospitali yetu,” akasema Dkt Ochieng’.
Tayari hospitali hiyo imetenga wadi ya wagonjwa wanaoshukiwa kuugua kipindupindu kutoka kaunti hiyo.
Mkurugenzi wa Afya ya Umma wa Kisumu Fred Aluoch awali alisema watu saba kutoka Rabuor walikuwa wamekimbizwa hospitalini humo baada ya kula chakula kibaya.
“Walikuwa wakiendesha majimaji na baadhi walitibiwa huku wengine wakilazwa hospitalini,” akasema Bw Aluoch.
Kutokana na mvua kubwa ambayo imekuwa ikishuhudiwa, wakazi wa Kisumu wameonywa wayatibu maji yao na kudumisha viwango vya juu vya usafi.
Tayari Mkurugenzi wa Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa Kaunti ya Kisumu Paul Oloo amesema mvua inayoshuhudiwa sasa huenda ikaendelea hadi mnamo Mei.
Kuzima kipindupindu, Bw Oluoch alisema wamekuwa wakisambaza dawa za kuyatibu maji kwa kusaidiana na wahudumu wa afya katika jamii.
Kando na Nyando, kaunti ndogo za Kisumu Mashariki, Muhoroni na Nyakach pia zinamulikwa na idara ya afya ili kuzima mkurupuko wa magonjwa yanayotokana na maji chafu .
“Tuko makini hasa Nyando na Muhoroni kwa sababu maeneo hayo mawili hutumia mto Nyando na Awasi. Kisumu Mashariki na Nyakach ambazo zinapakana na kaunti hizo ndogo pia zinafuatiliwa,” akasema Bw Oluoch.