Kimataifa

Aapa kuwashtaki wazazi wake kwa kumzaa bila idhini

February 6th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

MASHIRIKA Na PETER MBURU

MWANAMUME kutoka India amesema kuwa anapanga kuwashtaki wazazi wake kwa kumzaa bila idhini yake.

Raphael Samuel alisema kuwa ijapokuwa ana uhusiano mwema na wazazi wake, analinganisha suala la kupata watoto sawa na “utekaji nyara na utumwa.”

Samuel, ambaye ana miaka 27 na mkazi wa Mumbai amekuwa mwanaharakati mpinga uzazi, ambaye anashikilia imani kuwa si vyema kumleta mtoto duniani kuteseka kwa ajili ya wazazi kujiburudisha.

Muungano wa kupinga kuzaa unazidi kushika kasi India, huku vijana wakikaidi presha za wazazi kuwataka kutafuta vizazi.

Samuel alisema “Nawapenda wazazi wangu na tuna uhusiano mwema lakini walinileta kwa ajili ya kujiburudisha na furaha yao.”

“Maisha yangu yamekuwa mazuri lakini sioni sababu ya kuleta maisha mengine kupitia matatizo ya shule na kutafuta kazi, haswa kwa kuwa hawakutuma maombi waletwe duniani,” akasema jamaa huyo.

Samuel ana ukurasa wa Facebook unaoitwa Nihilanand ambao una mamia ya wafuasi, ambapo amekuwa akichapisha jumbe za kupinga hali ya watu kuzaa.

Katika chapisho moja, jamaa huyo anasema “sababu ya pekee ambayo inafanya watoto wako kupata matatizo ni kwa kuwa uliwazaa.”

“Kumleta mtoto duniani kwa nguvu, kisha kumlazimisha kupata kazi ni sawa na utekaji nyara na utumwa,” ujumbe mwingine unasema.

Baadhi ya wanaharakati wa kupinga uzazi India aidha wamehoji kuwa kuzaa kunasababisha upungufu wa rasilimali za dunia, hivyo watu wanafaa kujizuia kuendeleza vizazi kwa ajili ya kulinda mazingira.

Wanataja suala la kupata watoto kama kuchagia uharibifu wa mazingira na jamii kupoteza maadili.

“Kutoleta mtoto dunia hii ni njia moja ya kuhakikisha kuwa mtoto huyo hatateseka kamwe,” akahoji mwanaharakati mwingine.