Habari za Kitaifa

Ruto anavyouma Mlima Kenya huku akiipapasa 

Na MWANDISHI WETU April 3rd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

RAIS William Ruto anaonekana kuwa mwangalifu zaidi na anavyoshughulikia eneo la Mlima Kenya katika serikali yake, huku akiwafuta kazi baadhi ya viongozi na kuwateua wengine kutoka eneo hilo.

Hatua hii inaonekana kulenga kutuliza eneo hilo ambalo ni mojawapo ya maeneo yaliyochangia pakubwa ushindi wake katika uchaguzi wa 2022.

Rais alikasirisha eneo hilo baada ya kumtimua aliyekuwa naibu wake Rigathi Gachagua lakini akalipapasa kwa kumteua Profesa Kithure Kindiki kujaza nafasi hiyo.

“Hili sio eneo analoweza kupuuza kamwe hata kukiwa na mabadiliko ya kisiasa kama vile Serikali Jumuishi yake na kiongozi wa ODM Raila Odinga. Lazima afagie wale anaohisi wanaasi huku akiwateua wengine kutoka eneo hili ili kuondoa nembo ya usaliti. Ni mchezo wa kuuma na kupuliza wakati mmoja,” asema mchambuzi wa siasa Benard Kibara.

Katika mabadiliko ya hivi karibuni, Rais alifuta uteuzi wa aliyekuwa Katibu wa wizara Irungu Nyakera kuwa mwenyekiti wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Kenyatta (KICC) na akamteua Bw Samuel Waweru Mwangi kujaza nafasi hiyo.

Wiki jana, Rais Ruto alimfuta kazi Justin Muturi kama Waziri wa Utumishi wa Umma na nafasi yake ikatwaliwa na mbunge wa Mbeere Kaskazini Geofrey Ruku anayetoka Kaunti ya Embu anakotoka spika huyo wa zamani wa Bunge la Kitaifa.

Ruku anasubiri kupigwa msasa na bunge.

Alipomfuta kazi aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Mithika Linturi, alijaza nafasi yake na Dkt Andrew Karanja ambaye aliachishwa kazi rais alipounda Serikali Jumuishi na nafasi yake itachukuliwa na Bw Mutahi Kagwe. Wote hao wanatoka eneo la Mlima Kenya.

Katika Wizara ya ICT na Uchumi wa Kidijitali, aliyekuwa Waziri Dkt Margaret Ndung’u aliondolewa na nafasi yake ikachukuliwa na waziri wa sasa Bw William Kabogo.

Wachambuzi wa siasa wanasema mabadiliko haya yanatokana na siasa za ndani ya Mlima Kenya, huku Ruto akijaribu kuhakikisha kuwa anazidi kudumisha uungwaji mkono katika eneo hilo.

“Kuna tatizo la siasa za Mlima Kenya kwa kukosa chama chenye nguvu na umoja na ndilo Ruto anatumia kujinufaisha,” asema Kibara.

Aidha, wapo wanaoamini kuwa rais anajaribu kuhakikisha kuwa viongozi wote anaoteua ni wale waaminifu kwake na wanaomuunga mkono kwa dhati.

“Rais hataki ionekane kama Gachagua anasema ukweli anapodai Serikali inatenga eneo hilo. Hii ndio sababu akitimua mtu kutoka eneo hilo hasa wanaohusishwa na Wamunyoro (washirika wa Gachagua) anajaza nafasi yake na mtu kutoka eneo hilo anayehisi ni mwaminifu,” asema Kibara.

Anasema kwamba mabadiliko haya yanaweza kuwa na athari kubwa katika siasa za Mlima Kenya na kwa rais.

Baadhi ya viongozi hasa waliokuwa naye katika kampeni za uchaguzi uliopita kutoka eneo hilo wanaweza kuhisi kutengwa, hasa wale waliomuunga mkono Ruto tangu mwanzo.

Kwa upande mwingine, hatua ya kuwajumuisha viongozi wapya kutoka eneo hilo inaweza kumsaidia Rais kudumisha uungwaji mkono wake.

Jumatano, Aprili 2, 2025, Rais Ruto alifichua kuwa anazungumza na aliyekuwa Waziri Peter Munya na Bw Linturi, kuhusu uwezekano wao kurejea serikalini.

Ufichuzi huu ulifuatia ombi la Gavana wa Meru, Isaac Mutuma, ambaye alimrai Ruto wakati wa ziara yake ya maendeleo katika eneo la Mlima Kenya, kuwaingiza viongozi hao wawili kutoka Meru katika serikali jumuishi.

“Kuna viongozi wakuu hapa Meru, ambao hata ni wanachama wa Njuri Ncheke, na tunawaheshimu sana. Mmoja wao ni Peter Munya, na mwingine ni rafiki yako mkubwa, Francis Mithika Linturi. Katika hiyo serikali Jumuishi, ile inayowajumuisha marafiki wetu wote na viongozi kutoka kote nchini, Mithika Linturi na Peter Munya wanapaswa kuwa humo,” Mutuma alisema.

Ruto alijibu kwa kusema: “Gavana amenieleza kuwa kuna viongozi wawili kutoka eneo hili: Peter Munya na rafiki yangu Mithika Linturi. Viongozi hawa wawili tayari tunazungumza na tuna mpango. Tulieni, kila kitu kiko sawa.”