Habari za Kitaifa

Hofu Kahariri, Haji, Kanja wakishiriki siasa

Na MOSES NYAMORI April 4th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

HOTUBA ya Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja katika mkutano wa kisiasa wa Rais William Ruto akiwa Mlima Kenya imezua shutuma kali kutokana na kile kinachotajwa kama wakuu wa usalama kuingilia masuala ya kisiasa.

Bw Kanja ni afisa wa hivi karibuni wa usalama kuibua mjadala baada ya Mkuu wa Majeshi (CDF) Jenerali Charles Kahariri wiki iliyopita kuonya dhidi ya kampeni ya ‘Ruto Must Go’ – ‘Ruto lazima aondoke’.

Alisisitiza kuwa mabadiliko ya uongozi wa nchi yanapaswa kufanyika kwa mujibu wa Katiba.

Katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kieni, Kaunti ya Nyeri, Bw Kanja alihutubia wananchi akiwa katika sare rasmi za polisi.

Alikuwa ameandamana na Rais Ruto na Naibu Rais Kithure Kindiki.

Alipokaribishwa na Prof Kindiki, Bw Kanja aliuliza wananchi kwa lugha ya Kikuyu: “Je, mnafurahia kuwa na Rais hapa? Mngependa aje tena?”

Kauli hiyo ilitafsiriwa kama ishara ya kumuunga mkono Rais kisiasa, hali iliyozua mjadala mkali kuhusu nafasi ya polisi katika siasa za taifa.

Chama cha Mawakili Kenya (LSK) na viongozi wa kisiasa walilaani kitendo hicho, wakimtaka Bw Kanja aombe msamaha au ajiondoe kwenye wadhifa wake.

Rais wa LSK, Faith Odhiambo, alisema: “Tunamtaka Bw Kanja aombe radhi mara moja kwa tabia yake isiyofaa, ambayo inaweza kuhatarisha uadilifu wa Huduma ya Polisi.”

Aliongeza kuwa, kwa mujibu wa Ibara ya 245(1) ya Katiba, Inspekta Jenerali anapaswa kuwa huru na asifanye kazi kwa shinikizo ya mtu yeyote.

Msemaji wa Polisi, Muchiri Nyagah, alitetea Bw Kanja, akisema kuwa alikuwa akifanya kazi yake ya kusimamia usalama katika mkutano wa Rais.

“Inspekta Jenerali alikuwa Nyeri kwa sababu za kiusalama. Huduma ya Polisi haijawahi kupendelea upande wowote wa kisiasa,” alisema Bw Nyanga.

Naibu Gavana wa Machakos, Francis Mwangangi, aliongeza kuwa hakukuwa na tatizo lolote kwani Rais alikuwa kwenye ziara ya maendeleo.

“Hakuna sheria inayomzuia Inspekta Jenerali kuhudhuria hafla ya Rais. Ila, anapaswa kuhakikisha kuwa ofisi yake inasalia huru,” alisema Mwangangi.

Wiki iliyopita, Mkuu wa Majeshi, Jenerali Kahariri, pia alizua taharuki aliposema kuwa kampeni ya ‘Ruto lazima aondoke’ inapaswa kufanyika kwa mujibu wa Katiba.

Alisema haya wakati wa mhadhara ulioandaliwa na Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Ujasusi (NIS), Noordin Haji, ambaye alionya kuwa siasa za mgawanyiko zimeenea mitandaoni na zinatishia umoja wa kitaifa.

“Siasa za ukabila na mgawanyiko zinahatarisha uthabiti wa taifa letu,” alisema Haji.

Jenerali Kahariri aliongeza: “Hatuwezi kuruhusu vurugu za kisiasa zivuruge nchi. Serikali lazima iheshimiwe, na mabadiliko yafanyike kwa njia ya kikatiba.”

Miongoni mwa waliomkosoa Jenerali Kahariri ni Naibu Rais wa zamani Kalonzo Musyoka na Kiongozi wa People’s Liberation Party (PLP), Martha Karua.

Bi Karua alitaja matamshi ya Kahariri kama ukiukaji wa Katiba.

“Ni aibu kwa kiongozi wa majeshi kujiingiza katika siasa na kuwaelekeza Wakenya jinsi wanavyopaswa kutumia haki zao,” alisema.

Bw Musyoka naye alidai kuwa kauli hiyo ni njama ya kutisha wananchi.

“Serikali ya Ruto inataka kutumia majeshi kuzima uhuru wa kujieleza. Agizo la kutumwa kwa wanajeshi kuzima maandamano ya vijana lazima liondolewe mara moja,” alisema.

Aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, pia, alimtaka Jenerali Kahariri kutoshiriki siasa.

“Jeshi halipaswi kushiriki siasa. Tunapaswa kuheshimu Katiba,” alisema Gachagua.

Katibu Mkuu wa Jubilee, Jeremiah Kioni, alidai kuwa hatua ya Rais Ruto kutumia maafisa wa usalama kwa siasa ni ishara kwamba amepoteza uhalali wa kuongoza.

“Hii ni hali ya hatari ambapo taasisi huru zinaharibiwa na serikali ya Ruto. Polisi wameingizwa katika siasa baada ya machifu kukataa kutumiwa kwa kampeni,” alisema Kioni.

Mbunge wa Embakasi Central, Benjamin Gathiru, pia alionya kuwa hatua hiyo itaharibu uaminifu wa umma kwa polisi.