Watatu wafariki oksijeni ikikatika hospitalini
WATU watatu waliokuwa wamelazwa katika Hospitali Kuu ya Rufaa ya Pwani, Kaunti ya Mombasa walifariki baada ya hitilafu ya hewa oksijeni.
Watatu hao, Kimanzi Mwangi mwenye umri wa 81, Mariam Chai na Tito Mutua 45, walikuwa wamelazwa katika hospitali hiyo kufuatia matatizo mbalimbali ya kiafya.
Alfred Kimanzi mmoja wa familia ya Kimanzi alisema kuwa alipokuwa katika harakati za kuondoka hospitali ghafla alimuona babake akitapatapa kutafuta hewa.
Juhudi zake za kuwaita wauguzi kuja kumshughulikia hazikufaulu.
“Babangu alikuwa vizuri, baada ya kumpa chakula cha jioni nilijitayarisha kuondoka lakini ghafla baba akaanza kutapatapa. Nilijaribu kuwaita wauguzi lakini hawakuja, hatimaye alifariki,” alieleza Alfred.
Ilisemekana kuwa wodi zilizoathirika na mkasa huo; ni wodi ya tano, sita na ile ya watoto.
John Mutua, mwana mwingine wa Kimanzi, ameitaka serikali kuchukua hatua za haraka dhidi ya wale waliohusika na tukio hilo.
“Hii haikuwa ajali—hili ni tukio la uzembe lililosababisha vifo. Waliwezaje kukatiza oksijeni wakijua wazi kuwa maisha ya wagonjwa yaliitegemea? Walipaswa kuwa na mpango wa kuwahamishia wagonjwa kabla ya kufanya uamuzi huo,” alisema.
Mjane wa Kimanzi, Mbuthia Kimanzi, hakuweza kuficha majonzi yake.
Baada ya kusafiri mwendo mrefu kumtembelea mume wake, alishtuka kusikia kwamba alikuwa ameaga dunia hata kabla ya kupata nafasi ya kumuona kwa mara ya mwisho.
Familia zilizoathirika zinalalamika kuwa hata baada ya vifo hivyo, usimamizi wa hospitali umekaa kimya bila kutoa maelezo yoyote wala pole kwa waliopoteza wapendwa wao.
“Mpaka sasa, hakuna hata mtu mmoja kutoka kwa usimamizi wa hospitali aliyekuja kutufafanulia kilichotokea au hata kutuomba msamaha,” alisema Kennedy Mwilo, shemeji wa Tito Mutua.
Mwilo alieleza kuwa shemeji yake alilazwa Jumatano (Machi 26, 2025) iliyopita akiwa na matatizo ya kifua.
“Alikuwa akitegemea oksijeni, na sasa hayupo. Tunaomba serikali kuu iingilie kati na kuhakikisha haki inatendeka. Familia za waathiriwa waliokuwepo hospitalini walisema kuwa baada ya oksijeni kukatika, wauguzi walihangaika kusaidia wagonjwa, lakini walishindwa kuwahudumia wote.” Wakati vifo vilipotokea, wanadai kuwa wauguzi hao walitoweka, wakiwaacha jamaa wa marehemu kushughulikia miili ya wapendwa wao peke yao.
“Tulitumia kila kitu tulichoweza kumtunza baba yetu akiwa hai. Tulijitolea kwa hali na mali kuhakikisha anapata matibabu bora, lakini kwa uzembe wa watu wachache, maisha yake yakakatizwa ghafla,” alisikitika Kimanzi.
“Hili haliwezi kupita bila hatua kuchukuliwa.”
Maafisa wa polisi kutoka Kituo cha Tononoka walifika hospitalini kutuliza hasira za familia zilizoathirika.
Hata hivyo, hadi sasa, uongozi wa hospitali haujatoa taarifa rasmi kuhusu mkasa huo.
Juhudi za kuwasiliana na uongozi wa hospitali ili kupata kauli yao hazijazaa matunda.
Wakati huohuo, familia zilizopoteza wapendwa wao zimesisitiza kuwa hazitasita kutafuta haki, zikiitaka serikali kuhakikisha wahusika wanawajibishwa kisheria.
Kadri uchunguzi unavyoendelea, tukio hili la kusikitisha limezua maswali mapya kuhusu hali ya huduma za afya katika hospitali za umma, huku wengi wakitilia shaka ikiwa usalama wa wagonjwa unapewa kipaumbele cha kutosha.
Wakuu wa hospitali hiyo walidinda kutoa taarifa kuhusu vifo hivyo huku Gavana Abdulswamad Nassir akiahidi kuanzisha uchunguzi wa kina na kutoa ripoti kamili.