Habari za Kitaifa

Raila ‘ajivua’ nembo ya usaliti, asema ODM itagombea urais 2027

Na WINNIE ATIENO April 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KIONGOZI wa chama cha ODM, Raila Odinga anajitahidi kujivua nembo la usaliti kutokana na ndoa yake ya kisiasa na Rais William Ruto kwa kusisitiza kuwa chama chake kitakuwa na mgombeaji wa urais 2027.

Chama hicho kimetangaza kuwa kitawania urais katika uchaguzi mkuu wa 2027 kumenyana na Rais William Ruto.

Bw Odinga ana mkataba na Rais Ruto wanaosema ni wa kuunganisha taifa huku baadhi ya wandani wa waziri mkuu huyo wa zamani wakitangaza kuwa wataunga Ruto katika uchaguzi mkuu wa 2027.

Hata hivyo, Bw Odinga amejitetea akisema ushirikiano wake na Rais si usaliti kwa wakenya bali ulinuiwa kuleta amani wakati wa joto kali la kisiasa.“Hatujaingia katika ndoa hii na serikali ili kusaliti Wakenya.

Kenya ni muhimu sana kuliko watu binafsi. Lazima Wakenya waungane na wafanye kazi pamoja. Lakini wakati wa uchaguzi, ODM itakuwa debeni,” alielezea umma huko Mombasa Jumamosi.

Hii ni mara ya kwanza kwa Bw Odinga kutangaza rasmi hadharani kuwa chama chake kitawania urais katika uchaguzi mkuu ujao. Hata hivyo hakusema iwapo ni yeye atakayepeperusha bendera hiyo.

Ili kujitayarisha kwa kinyanganyiro cha uchakuzi mkuu miaka miwili ijayo, Bw Odinga alisema ODM itafanya uchaguzi wa chama katika sehemu zote nchini.

Aliwataka wagombeaji wote kuwa watulivu wakati wa uchaguzi huo ili kusizuke vurumai.“Nataka uchaguzi wa chama uwe wa kirafiki, msipigane. Atakayechaguliwa ni sawa kwani nyote ni ndugu,” alisema Bw Odinga.

Haya yanajiri siku chache baada ya wafuasi wa ODM huko Pwani kumtaka aahirishe uchaguzi wa chama wakihofia hakutakuwa na usawa na haki. Baadhi ya wanachama wa chama cha Chungwa katika Kaunti ya Mombasa wanataka uchaguzi wa mashinani wa chama uliopangwa kufanyika wiki ijayo uahirishwe kwa hofu ya kuwepo kwa udanganyifu.

Wanadai kuwa uchaguzi huo unapaswa kuahirishwa ili kutoa nafasi kwa mashauriano, wakihofia kuwa iwapo utaendeshwa katika mazingira ya sasa, huenda ukasababisha mgawanyiko ambao unaweza kudhoofisha umaarufu wa chama katika uchaguzi ujao.

Akizungumza kwa niaba ya wanachama wa chama hicho, James Owera aliibua tahadhari kuhusu madai ya kuingiliwa kwa uchaguzi wa mashinani na baadhi ya viongozi wa kisiasa, hali inayotilia shaka uhalali wa mchakato mzima.

“Hofu yetu kuu ni kwamba watu wanaoakisi sauti za mashinani si wale waliopendekezwa kushiriki uchaguzi. Wanaopendekezwa si maarufu miongoni mwa wananchi bali wanajulikana tu na uongozi wa chama,” alisema Owera.

Miongoni mwa wasiwasi walioueleza ni kuhusu vitendo vya kulazimisha na kutisha wapiga kura. Baadhi ya wanasiasa wanadaiwa kutumia mbinu za shinikizo, hila au hata vitisho ili kuwashawishi wanachama wa kuwachagua wagombea fulani.

Wakati huo huo kinara huyo wa ODM, alimtaka Rais kukabiliana na donda sugu la ufisadi na kuhakikisha wale wahusika wanachukuliwa hatua kali za kisheria.

Bw Odinga alisema kwenye mkataba wake na Rais Ruto walikubaliana kuimarishwa kwa ugatuzi hasa katika sekta ya afya na elimu.“Serikali za kaunti zinafaa kufanya kazi kisawasawa.

Ufisadi ni adui ya wakenya, pesa nyingi zinaenda kwa mifuko ya watu binafsi tunataka wahusuka wakamatwe na kushtakiwa,” alisema Bw Odinga